Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu imetupilia mbali pingamizi la upande wa utetezi katika kesi ya ugaidi inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe na wenzake.
Pingamizi lililotupwa ni kuhusu madai ya mshtakiwa wa Pili katika kesi hiyo, Adam Kasekwa kwamba alichukuliwa maelezo ya onyo nje muda, pia aliteswa kabla kabla ya kuandika maelezo hayo.
Uamuzi huo umetolewa na Jaji Kiongozi Mustapha Siyani ambapo amesema baada ya kusikiliza hoja za mawakili na mashahidi watatu watatu wa kila Upande, amebaini ushahidi wa Upande wa utetezi hauendani na mapingamizi yao.
“Ninao mapingamizi mawili ya utetezi waliyoyaibua hayana nguvu wala mashiko, kwani ushahidi walioutoa hauendani na mapingamizi waliyoyawasilisha, hivyo nakipokea kielelezo cha Shahidi wa Pili, ACP Ramadhan Kingai,” Jaji Kiongozi Siyani.
Kutokana na kupokelewa kwa kielelezo hicho, kesi hiyo itaendelea katika ngazi ya kesi ya msingi ambapo iliishia kwa Shahidi wa Pili wa Jamhuri, ACP Ramadhan Kingai.
Mbali na Mbowe na Kasekwa, washitakiwa wengine ni Mohamed Ling’wenya na Alfan Bwire ambao wanakabiliwa na mashitaka 6 ikiwemo mawili kula njama, kutenda makosa ya Ugaidi, kukutwa na mali iliyokusudiwa kutumika kutenda vitendo vya kigaidi na kufadhiri vitendo vya Kigaidi (Mbowe).