Rais wa Wataalamu wa Macho Tanzania, Eden Mashayo amesema watu wanaovaa miwani kiholela na kubandika kope wako hatari kupata matatizo ya macho.
Mashayo aliyasema hayo jana wakati wa zoezi la upimaji macho katika Stendi kuu ya Mabasi yaendayo Mikoani ya Magufuli jijini Dar es Salaam Ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Wiki ya Afya ya macho.
Alisema ni muhimu watu kukutana na wataalamu wa afya na kupima macho kabla ya kuvaa miwani hata za urembo.
“Vitu hivyo vyote vinahitaji kumuona mtaalamu hata kubandika kope sio vizuri ni muhimu watu waangalie afya ya macho yao wasipuuzie,” Eden
Alieleza kuwa takwimu zinaonesha kuwa asilimia moja ya watanzania ni vipofu huku wengine asilimia 55 wakiwa na tatizo la uoni hafifu.
“Asilimia 20 ya Wananchi wanahitaji huduma ya macho na wengi wanaopata matatizo ya macho yanatibika, lengo letu la kufika hapa ni watu kupima afya ya macho,” Eden
Mashayo alisema sababu za kuchagua Stend ni kuwapa nafasi ya madereva kupima kwani uoni hafifu unaweza kuwa chanzo cha ajali za barabarani.
“Hivyo endapo dereva atagundulika na kutibiwa itasaidia kupunguza ajali na kwa wale wanaotoa leseni ni muhimu kuwahimiza madereva kupima afya ya macho angalau mara moja kwa mwaka” Eden
Kwa upande wake Mratibu wa Afya ya Macho Mkoa wa DSM, Dk Patrick Kabangut’se alibainisha kuwa asilimia mbili ya watu wanaofika kwenye huduma wanagunduliwa kuwa na matatizo ya macho kwa mkoa huo.
” Wengi wanatatizo la macho kutokana na sababu mbalimbali wengi hawafiki kwasababu ya gharama na uelewa mdogo hivyo huduma hii inasaidia sana” Dkt. Patrick Kabangut’se
“Hata madereva wengine wanaendesha magari bila kujua kama wanashida ni watu wengi wanahitaji huduma ,wito wangu watu wajitokeze kupima macho katika huduma hizi na pia hospitali zetu za Wilaya na Mkoa,” Dkt. Patrick Kabangut’se
Naye Mtaalamu wa macho kutoka Taasisi ya Vision Care Eyes Clinic Careen Mashayo alisema wanatarajia kupima watu 300 katika huduma hiyo ya siku moja.
“Hadi sahizi saa nne asubuhi tumepima watu zaidi ya 100 na watu 80 wamekutwa na tatizo mpaka jioni tutakuwa tumefikia lengo na kuvuka” Careen
Alisema matumizi ya muda mrefu ya Simu na Compyuta yanaweza kusababisha matatizo ya macho.