Wizara ya Viwanda na Biashara imewajengea uwezo wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira na Kamati ya Kudumu ya Baraza la Wawakilishi la Kilimo, Biashara na Utalii kuhusu Mkataba wa Eneo Huru la Biashara Afrika (AfCTA).
Wajumbe hao wamejengewa uwezo huo kupitia semia iliyowakutanisha wajumbe wa kamati hizo iliyofanyika Leo tarehe 12 mwaka 2021 jijini Dodoma ikiwa ni hatua ya Wizara katika kutekeleza mkakati wa kujenga uwelewa wadau kuhusu mkataba huo.
Aidha, katika nyakati tofauti wajumbe wa Kamati hizo wametoa maoni na kutaka wafanyabiashara kuchangamkia fursa za biashara wakati wa kutekeleza mkataba huo utakapoanza ikiwemo uondoaji wa viwakzo vya kibiashara, uzalishaji wa bidhaa zenye ubora, usafirishaji wa bidhaa, kodi, na sheria mbalimbali zinazohusika na biashara pamoja na kuzingatia, kulinda na kuweka maslahi ya Taifa mbele wakati wote wa utekelezaji wa mkataba huo.
Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara Prof. Kitila Mkumbo (MB), Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt. Stergomena Tax amesema Serikali imejiandaa kikamilifu katika kutekeleza Mkataba huo ambao utachangia kukua kwa uchumi hapa nchini.
Alisema Serikali imeweka mikakati mbalimbali ya utekelezaji wa mkataba ambao una fursa nyingi za kukuza na kuendeleza biashara Tanzania na utawawezesha watanzania kunufaika na fursa za eneo huru la biashara Afrika ikiwemo kuongeza uwekezaji na uzalishaji viwandani Ili kukidhi mahitaji ya soko kubwa jipya la Afrika.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Kamati ya Kilimo, Biashara na Utalii ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mhe. Yussuf Hassan Idd ametoa rai kwa Serikali kujipanga kutumia fursa zinazopatikana kutokana na maktaba huo huku ikizingatia utofauti wa uchumi kati ya nchi wananchama wa bara la Afrika wanaotekeleza mkataba huo.
Awali akimkaribisha Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt. Tax, Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Bw. Doto James amesema Tanzania imeridhia na Mkataba huo ambao unafaida nyingi kwa taifa ikiwemo upatikanaji wa soko kubwa la bidhaa na huduma lenye idadi ya watu takriban bilioni 1.2.na utasaidia kuongezeka kwa tija na ubora kwa bidhaa na huduma za Tanzania kutokana na kuongeza kwa ushindani na hivyo kupelekea kupungua kwa bei za bidhaaa.
Awali, akitoa mada kwenye semina hiyo, Mkurugenzi wa Mtangamano wa Biashara Wizara ya Viwanda na Biashara Bw. Ali Gugu amesema Tanzania imekuwa nchi ya 41 kuridhia Mkataba AfCFTA na itanufaika fursa zote za kibiashara zinazotokana na Makataba huo ikiwemo kupatikana kwa masoko mapya ya mazao ya kilimo yatakayochochea uzalishaji, kuimarika kwa mnyororo wa thamani wa mazao ya kilimo yanayohusisha wakulima wadogo.
” Uzuri wa mkataba huu una kifungu ambacho kinaonesha nchi mwanachama hailazimishwi kutoa taarifa ambazo zitakinzana na utekelezaji wa sheria au kwenda kinyume cha matakwa ya nchi na pia inatoa fursa ya nchi kutowajibika kutoa taarifa ya maandishi baada ya miaka mitano ya utekelezaji wa mkataba.”
Bw. Ali Gugu amesema Tanzania imekuwa nchi ya 41 kuridhia Mkataba AfCFTA ambao hadi sasa hadi sasa jumla ya nchi 54 kati ya nchi 55 wanachama wa Umoja wa Afrika zimesaini Mkataba huo ulianza kutekelezwa rasmi tarehe 30 Mei, 2020. Jumla ya nchi 41 kati ua 55 zimeridhia Mkataba huo na zimewasilisha mapendekezo ya tariff offer kwa ajili ya kuanza kufanya biashara. Kati ya nchi hizo, zipo jumuiya nne (4) za Umoja wa Forodha ambazo ni Jumuiya ya Afrika mashariki (EAC), Jumuiya ya Uchumi ya Nchi za Afrika ya Kati (CEMAC), Jumuiya ya Uchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) na Umoja wa Forodha Kusini mwa Afrika (SACU).
Akielezea faida za Mkataba huo Bw. Gugu amesema Tanzania itanufaika fursa zote za kibiashara zinazotokana na Makataba huo ikiwemo kupatikana kwa masoko mapya ya mazao ya kilimo yatakayochochea uzalishaji, kuimarika kwa mnyororo wa thamani wa mazao ya kilimo yanayohusisha wakulima wadogo kama vile alizeti, pamba, karafuu, viungo, matunda na mbogamboga kutokana na kuongezeka kwa soko la bidhaa zitakazozalishwa nchini na kuongezeka kwa uzalishaji na ajira kwa wakulima na wadau wanaohusika katika mnyororo wa thamani wa mazao ya kilimo.
Ameongeza kuwa Mkataba wa AfCFTA umezingatia maslahi mapana ya nchi wanachama kama Kuvilinda viwanda vichanga, Usalama wa chakula, Upotevu wa mapato ya serikali, Sekta zinazozalisha ajira kwa watu wengi, Sekta za kimkakati na Uhuru wa kisera mambo ambayo yatafanya kila mwanachama kuwa mnufaika katika mkataba huu.
Pamoja na hayo ameongezea faida mbalimbali zitapatikana kwa nchi ambazo zitaridhia mkataba huu kuwa ni pamoja na kuingiza biashara zao katika nchi wanachama bila kutozwa kodi kubwa ya ushuru katika bidhaa zinazozalishwa ndani ya bara la Afrika kwa 97% Ndani ya miaka kumi ijayo ikiwa ni makubaliano ya wakuu wa nchi za Bara la Afrika.
Faida nyingine za kuridhia mkataba huo ni pamoja na na Kuimarisha ushirikiano wa kibiashara sambamba na kuviendeleza viwanda na wajasiriamali kundi la Wajasiriamali wodogo sana, Wadogo na wa Kati (MSMEs), Upatikanaji wa bidhaa za aina mbalimbali (varieties) nchini na Uhawilishaji wa teknolojia kutoka nje ya nchi (technology transfer) kutokana na uwekezaji utakaofanyika nchini.
Eneo Huru la Biashara la Afrika (African Continental Free Trade Area-AfCFTA) ni utaratibu wa pamoja wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika unaolenga kuchochea uchumi na Biashara miongoni mwa nchi wanachama, kuongeza Pato la Taifa la jumla ya zaidi ya Dola za Kimarekani trilioni 3.4 na fursa za uchumi unaokua kwa kasi na kuongeza mchango wa Afrika kwenye soko la dunia kwa asilimia 2.8 huku sekta za kilimo, chakula na huduma zikipewa nafasi kubwa katika ukuaji huo
Lengo hilo litafikiwa kwa kufunguliana masoko ya biashara ya bidhaa na huduma kwa kuondoleana ushuru wa forodha (tariff) na kulegezeana masharti na taratibu nyingine zisizokuwa za kiushuru. Aidha, utaratibu huo unalenga kufanya Bara la Afrika kuwa Soko Moja ambapo nchi hizo zitaweza kutangamanisha juhudi nyingine za mtangamano wa kibiashara na uchumi ambazo nchi wanachama wa Umoja wa Afrika zimeshaanzisha.