Mfanyabiashara maarufu nchini, James Rugemalira leo Novemba 16, 2021 amerudi tena katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa ajili ya kufatilia mwenendo wa kesi yake aliyoifungua mahakamani hapo dhidi ya watuhumiwa 11.
Rugemalira aliyesota gerezani kwa miaka minne na miezi mitatu, katika watuhumiwa hao 11 zikiwemo taasisi za fedha na watu binafsi anaowatuhumu kuisababishia Serikali hasara ya Sh.Trilioni 61.
Kesi ya Rugemalira ipo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shahidi ambapo hata hivyo haikuweza kuendelea leo na imeahirishwa hadi Novemba 30, mwaka huu.
Miongoni mwa wajibu maombi ambao Rugemalira anawatuhumu ni Benki ya Standard Chartered (Hong Kong), Benki ya Standard Chartered Tanzania, Benki ya Standard Chartered (Malaysia) Berhad, Wartsila Netherlands B.V na Wartsila Tanzania Limited.
Rugemalira na mwenzake Harbinder Singh Seth, walipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Kisutu Juni 19, mwaka 2017 wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi iliyokuwa na mashtaka 12 kabla ya kuongezwa aliyekuwa mwanasheria wa IPTL, Joseph Makandege.
Kesi hiyo ilitokana na kashfa ya uchotaji wa mabilioni ya pesa katika akaunti ya Tegeta Escrow iliyokuwa imefunguliwa Benki Kuu kutokana na mgogoro wa malipo ya gharama za uwekezaji kati ya IPTL na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) lililopinga malipo hayo kuwa yalikuwa makubwa.