Serikali imesema kuwa kupanda kwa bei za Saruji katika kipindi cha mwezi September -November 2021 kulisababishwa na mfumo wa usambazaji wa bidhaa hiyo na hautokani na kupanda kwa gharama za uzalishaji viwandani kwa sababu hiyo ongezeko la bei ya saruji linachukuliwa kuwa halikuwa halali.
Kwa upande wa ongezeko la bei za bidhaa zinazotokana na malighafi ya vyuma (Mabati na nondo) Serikali imesema kupanda kwa bei hiyo kulitokana na kupanda kwa bei za malighafi kutoka nje ya nchi kwa kuwa malighafi za bidhaa hizo kutoka ndani hazitoshelezi.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Prof. Kitila Mkumbo wakati akizungumzia tathmini iliyofanywa kuhusu mwenendo wa uzalishaji, usambazaji na bei za vifaa vya ujenzi hususan saruji, mabati na nondo katika mikoa tisa kwa kipindi cha mwezi September -November 2021 katika mikoa ya Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Kilimanjaro, Mbeya, Mwanza, Pwani, Shinyanga na Ruvuma.
Waziri Mkumbo amesema bei za Saruji zimepanda kwa wastani wa shilingi 1,000. kwa upande wa Mabati matokeo ya tathmini yanaonyesha kuwa bei ya mabati imepanda kwa wastani wa asilimia 5.5 kwa mfano Mwanza imepanda kutoka shilingi 31,700 hadi shilingi 33,400, Dar es salaam bei imepanda kutoka shilingi 28,000 hadi 29,000.
Akizungumzia hatua mbalimbali zilizochukuliwa na Serikali katika kukabiliana na upandaji usiohalali wa bidhaa muhimu nchini Waziri Mkumbo amehihimiza tume ya ushindani kufuatilia kwa karibu mwenendo wa upangaji bei nchini na kuwachukulia hatua stahiki za kisheria wafanyabiashara ambao wanakiuka sheria ya ushindani nchini aidha ameahidi kurekebishwa kwa sheria na kanuni mbalimbali ili kuruhusu kuingizwa kwa urahisi zaidi malighafi zinazohitajika katika uzalishaji wa bidhaa za vyuma ikiwemo kuruhusu kuingizwa kwa vyuma chakavu kutoka nje kwa utaratibu utakaohakikisha kuwa bidhaa hiyo inapatikana nchini lakini bila kuathiri afya ya mazingira ya nchi yetu.