Wanafunzi watatu wameuawa na wengine wanane kujeruhiwa akiwemo mwalimu mmoja katika shambulizi la risasi katika shule ya sekondari katika jimbo la Michigan nchini Marekani.
Maafisa wanasema waliyofariki ni mvulana wa miaka 16 na wasichana wawili wa miaka 14 na 17. Polisi wanadai mshukiwa, mwanafunzi wa shule hiyo, alitumia bunduki ambayo baba yake alinunua siku zilizopita.
Wanafunzi wameelezea kujificha chini ya madawati wakati wa shambulio hilo. Wengine walikuwa wamesalia nyumbani Jumanne kwa sababu ya wasiwasi wa usalama.
Polisi walipokea simu za dharura kutoka kwa shule ya sekondari katika mji wa Oxford, takriban maili 40 (65km) kutoka Detroit na ndani ya dakika chache, maafisa walikuwa wamepokea simu 100 kwa namba 911, Afisa Msaidizi wa Kaunti ya Oakland Mike McCabe aliwaambia waandishi wa habari.
Maafisa wanasema mshukiwa, mvulana mwenye umri wa miaka 15, alijisalimisha dakika tano baada ya polisi kuitwa.
Hakuna risasi iliyofyatuliwa wakati wa kukamatwa na kijana huyo hakujeruhiwa, McCabe aliongeza kwamba mvulana huyo alikuwa darasani kabla ya ufyatuaji risasi kuanza. Mkuu wa polisi wa kaunti ya Oakland, Mike Bouchard, alisema maafisa wake walimkamata mpiga risasi huyo akiwa bado na risasi saba kwenye bunduki.