Katibu Tawala Mkoa wa Dar es Salaam Hassan Rugwa ametoa wito kwa Wakurugenzi na Mameya wa Halmashauri za jiji la Dar es Salaam, kuongeza idadi ya huduma za maegesho ya vyombo vya usafiri kwenye hifadhi za barabara, ili kuongeza wigo wa ukusanyaji mapato kwa serikali za mitaa.
Katibu Rugwa ametoa rai hiyo leo jijini Dar es Salaam, katika kikao cha makabidhiano ya jukumu la ukusanyaji ushuru wa maegesho ya vyombo vya moto kwenye hifadhi za barabara, kutoka Wakal la wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) kwenda kwa mamlaka za serikali za mitaa ambapo amewataka kuwa wabunifu katika utoaji huduma hiyo.
Kwa upande wake Meneja wa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini Tarura Mkoa wa Dar es Salaam Geofrey Mkinga amesema TARURA imekabidhi jumla maengesho 14,740 pamoja na kanuni za serikali za mitaa katika kuhakikisha zoezi hilo linaendelea vyema, kwakuwa ni moja ya chanzo cha Mapato ya Serikali na kinachochangia ukarabati na ujenzi wa miundombinu ya barabara Vijijini na Mijini ambayo ni jukumu kuu la TARURA.
Aidha Mkinga amesema katika shughuli za ukusanyaji ushuru wa maegesho miongoni mwa changamoto zilizokuwa zinakabili shughuli hizo ni pamoja ni wananchi kutokuwa na uelewa mpana namna mfumo unavyofanya kazi huku nguvu kubwa ikiwa utoaji elimu kwa umma kwa muda wa miezi sita ili kutambua mfumo unavyofanya kazi.