Uchawi si neno geni katika jamii zetu, wengi wetu tumekuwa tukihusisha na imani za kishirikina na kupelekea madhara mbalimbali kutokea miongoni mwa watu walio na imani juu ya suala hilo.
Chuo Kikuu cha Dar es salaam kupitia Idara ya Sosholojia kimeendelea kufanya utafiti juu ya nadharia hizo na namna ambayo itasaidia kupunguza madhara kwa jamii yatokanayo na imani juu ya mambo ya kishirikina.
Dr Richard Sambaiga ambaye ni Mhadhiri mwandamizi chuo kikuu cha Dar es salaam, idara ya Sosholojia na Anthropolojia ameeleza juu ya warsha iliyofanyika katika Chuo Kikuu cha Dar es salaam ambayo imelenga namna ya kuzuia madhara yanayotokana na imani na vitendo vya kishirikina nchini Tanzania.
Warsha hiyo ni sehemu ya mradi wa miaka miwili unaoshirikisha taasisi ya African Caribbean Institute kutokea nchini Marekani na Chuo Kikuu cha Dar es salaam katika kufanya tafiti na kutoa takwimu za kisayansi juu ya hali halisi ya uchawi ili kuja na mikakati ya kuzuia mauaji na vurugu zinazotokana na imani za kishirikina.
Utafiti huo unaofanywa juu ya uwepo wa imani za kishirikina umetokana na wimbi la mauaji miongoni mwa wanajamii ambapo majibu yatayopatikana yatajibu maswali mbalimbali juu za juu ya ukweli uliopo kuhusu imani hizo.