Miili ya marehemu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), sasa itapelekwa chumba cha kuhifadhia maiti kwa gari la wagonjwa Ambulance’, badala ya utaratibu wa kutumia vitanda.
Akizungumza Dar es Salaam Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Prof Mohammed Janabi, wakati alipokuwa anawaaga wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), alisema mabadiliko mengine ni wagonjwa wanaotolewa katika kitengo cha dharura watabebwa na Ambulance kupelekwa wodini.
“Ambalo tumeanza nalo leo ni kwamba bahati mbaya ikitokea mgonjwa amefariki mwili wa marehemu utachukuliwa na Ambulance kwenda kuhifadhiwa chumba cha kuhifadhi maiti, Wagonjwa waliotoka kitengo cha dharura watakuwa wanabebwa na gari la kubebea wagonjwa kupelekwa wodini” Janabi
“Kwa sababu ni hospitali kubwa, kwanza tutaanza kuboresha kwa wafanyakazi, itakuwa rahisi mwili kubebwa na Ambulance, kuliko kusukuma, kukiwa na vifo, mwili mmoja uko Kibasila, mwingine uko Sewahaji wanachoka wafanyakazi. Pia kutoa heshima kwa marehemu tunawahifadhi kwa njia hiyo,” amesisitiza Prof Janabi.
Amesema miongoni mwa vipaumbele vyake ni kuboresha huduma za afya na kuiendekeza Muhimbili kuwa hospitali ya Taifa.