JESHI la Polisi mkoani Mbeya limemkamata mchimbaji na mnunuzi wa madini, Ezekiel Luhwesha (31) akituhumiwa kumuua wakala wa maegesho ya magari jijini Mbeya, William Mgaya (58).
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga alisema Luhwesha ambaye ni mkazi wa wilayani Chunya mkoani Mbeya, anatuhumiwa kumuua Mgaya Novemba 26 saa 4:30 asubuhi katika eneo la Mafiati kata ya Ruanda kwenye ofisi za Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (Tarura) jijini humo.
Kamanda Kuzaga alisema jana kuwa siku ya tukio, Mgaya na mwezake Almasi Shaban (32) wote wakala wa maegesho ya magari,wakiwa katika kazi yao ya kukusanya ushuru walimkamata Ezekiel baada ya kuscan namba ya gari lake T 772 DVY Toyota Hilux.
Ilidaiwa kuwa gari lilikuwa likidaiwa Sh 7,500 na mtuhumiwa alitakiwa kulipa deni hilo lakini alihitaji kuhakiki deni hilo hivyo waliongozana hadi ofisi za Tarura.
“Baada ya kuoneshwa taarifa katika mfumo, mtuhumiwa aliliridhika na kuahidi kulipa deni hilo,lakini wakala Willium Mgaya alimtaka kulipa deni hilo papo kwa hapo kwa sababu deni hilo ni la muda mrefu na ndipo yalitokea majibizano yasiyo rafiki kati yao na kupelekea mtuhumiwa kutoa pisto yake na kumfyatulia risasi kifuani Willium Mgaya na kupoteza maisha muda mfupi baada ya kufikishwa hospitali ya rufaa Mbeya kwa matibabu,”alisema Kamanda Kuzaga.
Alisema mtuhumiwa yupo polisi na silaha yake aina ya bastola yenye namba T.0620-19J0037 ikiwa na risasi tisa ndani ya magazini inashikiliwa.
Kamanda Kuzaga alihimiza wamiliki wa silaha za moto wazingatie masharti ya umilikishwaji kama walivyoomba na wasizitumie tofauti na masharti yalivyoeleza ikiwa ni pamoja kujichukulia sheria mkononi.