Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano ambaye pia ni Mbunge wa Mbeya Mjini, Mhe. Dkt. Tulia Ackson leo Januari 9, 2023 amefanya ziara ya kuzitembelea kaya zilizoathirika na mafuriko yaliyosababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha Jijini humo.
Katika ziara hiyo Dkt. Tulia amejionea athari ya mvua hiyo ikiwemo uharibifu wa miundombinu, nyumba na mali mbalimbali za wananchi katika maeneo ya Kata za Igawilo, Uyole, Iganjo na Iduda.
Dkt. Tulia amewapa pole wahanga wa mafuriko hayo na kuwaahidi kwamba atashirikiana na Serikali kuhakikisha wanaboresha miundombinu ya Jimbo hilo ili kuwezesha kupunguza athari kama hizo zisijitokeze tena.
Pamoja na mambo mengine Dkt. Tulia ametoa msaada kilo 800 za mchele na kilo 200 za maharage kwa wahanga hao huku akiahidi kushirikiana na mamlaka za Serikali na wadau ili kufanikisha upatikanaji wa misaada zaidi.
“Ndugu zangu niwape pole sana kwa haya maswahibu yaliyowakuta, niwahakikishie Serikali yenu tukufu ipo nanyi katika kipindi hiki na nimeongea na Mheshimiwa Waziri Mkuu kumuelezea haya na amenihakikishia kwamba watakuja kufanya tathimini ili kuona hatua ya kufanya ili kukabiliana na janga hili” Amesisitiza Dkt. Tulia