Zaidi ya Wakuu wa Shule na walimu wakuu 40 wameondolewa katika nyadhifa zao katika mkoa wa Kagera baada ya shule tano za msingi kufutiwa matokeo ya mtihani wa taifa wa kuhitimu darasa la saba mwaka jana
Huu ni utekelezaji wa agizo la Waziri ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa – TAMISEMI Angellah Kairuki alilolitoa kwa Mkuu wa Mkoa huo Albert Chalamila
Akizungumza katika kikao kazi cha tathimini ya utelekezaji wa mkakati wa elimu na uwekaji wa mpango kazi wa utekelezaji kwa mwaka 2023 kilichoendeshwa na waziri wa TAMISEMI Angellah Kairuki, Chalamila amesema kuwa utaratibu wa kuondoa watumishi wasio waadilifu hasa katika sekta ya elimu unaendelea
“Nadhani mkoa wa Kagera uliongoza kwa shule nyingi kufutiwa, katika asilimia 100 sisi tulikuwa na asilimia 25, maana yake kulikuwa na ishara za udanganyifu, na wewe ulinielekeza mimi kwa ukali mkubwa sana kwamba kama kuna walimu wanahusika katika udanganyifu huo waondolewe kwenye nyadhifa zao, ili wengine waingie na mkoa uweze kupata maendeleo, hili limefanyika na linaendelea” Chalamila.
Kwa upande wake Waziri wa TAMISEMI Angela Kairuki amewataka viongozi katika nafasi zao kuimarisha uwajibikaji wa watumishi ili kuleta tija katika sehemu zao za kazi, lakini pia akasisitiza kuondoa utoro wa wanafunzi na walimu ambao ni viongozi huku mahudhurio yao kazini yakiwa ni hafifu.
“Zipo tuhuma wapo walimu na wapo viongozi wengine katika sekta zetu ni walevi, na baadhi yenu wanakunywa pombe saa za kazi, yaani wanaonekana katika vilabu vya pombe muda ambao wanapaswa kuwa kazini, hili likome mara moja” Kairuki.
Nao baadhi ya washiriki wa kikao hicho wameiomba serikali kuendelea kuondoa changamoto zinazoikabili sekta ya elimu, ili kuweka mazingira bora ya kujifunzia na kufundishia, kwa lengo la kuinua kiwango cha ufaulu.