Mamlaka ya Makumbusho ya mjini Berlin imesema iko tayari kuyarudisha mamia ya mafuvu ya vichwa kutoka nchi za Afrika Mashariki zilizokuwa chini ya ukoloni wa Ujerumani hii ni baada ya kufanya utafiti kwa miaka kadhaa na kutambua asili yake.
DW Kiswahili inaripoti kuwa utafiti huo ulifanyiwa mafuvu zaidi ya elfu moja ambapo 904 kati ya hayo huenda yakapelekwa Rwanda, 202 Tanzania na 22 nchini Kenya ambapo Watafiti hawakuweza kutambua asili ya mafuvu mengine saba.
Kulingana na Wakfu wa Urithi wa Kitamaduni wa Prussia, idadi kubwa ya mafuvu hayo yalitolewa makaburini ila baadhi yalitoka sehemu zilizokuwa zikitumiwa kufanya mauaji na baadhi yalitokana na mauaji yaliyofanywa na Wajerumani kipindi cha ukoloni.