Wanasheria wa Usain Bolt, mmoja wa Wanariadha wakubwa zaidi duniani, wamesema mapema wiki hii kwamba zaidi ya Dola Milioni 12.7 (TZS Bilioni 29.65) hazionekani kwenye akaunti ya Mwanariadha huyo na kampuni ya kibinafsi ya uwekezaji nchini Jamaica ambayo Mamlaka inachunguza.
Wakili Linton P. Gordon alilipatia Shirika la Habari la The Associated Press nakala ya barua iliyotumwa kwa kampuni ya Stocks & Securities Limited ikitaka pesa hizo zirudishwe, Gordon alisema akaunti ya Bolt ilikuwa na Dola Milioni 12.8 lakini sasa ina salio la $12,000 (Tzs Milioni 28) pekee.
Pesa za kwenye akaunti ya Bolt zilikusudiwa kutumika kama pesa za pensheni kwa Mwanariadha huyo na kwa Wazazi wake.
Bolt anajulikana kama mmoja wa Wanariadha bora zaidi duniani na akishikilia rekodi za dunia katika mbio za relay za mita 100, 200 na 4×100, Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 36 alistaafu mwaka wa 2017 huku akiwa na mikataba mingi ya udhamini na makampuni kama puma yenye faida kubwa, ikisadikiwa kumlipa Dola Milioni 4 kwakuvaa tu bidhaa zao.