Chelsea wamekubali kutoa kiasi cha kuvunja rekodi ya Uingereza cha euro 121m (£107m) kwa kiungo wa Benfica wa Argentina Enzo Fernandez.
Mkataba huo unapita kiasi cha £100m ambacho Manchester City walilipa kwa Jack Grealish mwaka 2021.
Benfica ilisema katika taarifa yake “imefikia makubaliano na Chelsea FC kwa uuzaji wa haki zote za mchezaji Enzo Fernandez”.
Fernandez, ambaye alijiunga na Benfica pekee kwa dau la pauni milioni 10 mwezi Agosti, alitawazwa mchezaji chipukizi bora wa michuano hiyo wakati wa ushindi wa Kombe la Dunia la Argentina nchini Qatar.
Kuwasili kwa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 22 kunaifanya Chelsea kutumia Januari hadi £288m, kulingana na tovuti ya uhamisho ya Transfermarkt.
Hiyo inafuatia gharama ya £292m msimu wa joto – rekodi kwa klabu ya Uingereza katika dirisha la majira ya joto.
Huu ni usajili wa sita kwa bei ghali zaidi wa muda wote, sawa na euro 120m ambayo Barcelona ililipa kwa fowadi wa Ufaransa Antoine Griezmann mnamo 2019.