Serikali imesema hadi kufika mwaka 2025 huduma ya maji safi na salama katika mkoa wa Manyara inatarajiwa kuwafikia wananchi kwa asilimia 85.
Mkuu wa Mkoa wa Manyara Charles Makongoro Nyerere amesema hayo wakati akishuhudia utiaji saini wa mikataba ya miradi ya maji katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Manyara kati ya Wakala wa maji safi na usafi wa mazingira (RUWASA) na wazabuni waliopata tenda ya kutekeleza miradi hiyo ya maji uliofanyika katika ofisi za mkuu wa mkoa wa Manyara.
Miradi inayotarajiwa kutekelezwa na wakandarasi waliosaini mikataba ni miradi 28 ambapo miradi 7 ni mipya, miradi 8 ya kuongeza mitandao, visima 26 na usanifu wa miradi 53 kwa ujumla utekelezaji wa miradi hiyo utagharimu kiasi cha shilingi bilioni 15 na milioni 406 ambazo tayari zimetolewa na serikali ya jamhuri ya muungano wa Tanzania.
Nae Meneja wa RUWASA Mkoa wa Manyara Mhandisi Walter Kirita amesema kwa sasa wanahudumia asilimia 80 ya wakazi wa mkoa wa Manyara hasa waliopo vijijini na huduma ya maji imefikia asilimia 64.3 sawa na ongezeko la asilimia 3.3 kutoka asilimia 61 mwezi juni mwaka 2022 ambapo takwimu za utoaji wa Maji Mkoa wa Manyara ikiwa asilimia 63 wilaya ya Hanang , Babati asilimia 76, Kiteto asilimia 60.9, Mbulu asilimia 65.2, Simanjiro 51.6
Nao wakandarasi na wazabuni wamesema wapo tayari kufanya kazi kwa bidii kama mikataba inavyoeleza kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati ili wananchi waweze kupata huduma ya maji safi na salama.