Spika wa Bunge, Dr Tulia Ackson ameagiza kauli ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dr. Mwigulu Nchemba kufutwa kwenye kumbukumbu rasmi za bunge kwa kuwa kauli hiyo haikujielekeza kwenye kujibu hoja badala yake alishughulika na mtu binafsi.
Dr. Tulia Ackson amesema hii inatokana na wabunge wakiwa wanachangia wanashugulika na mtu binafsi badala ya hoja hivyo Waziri au Naibu Waziri anapojibu analazimika kumjibu mtu badala ya hoja alizozisema hivyo amewaomba pande zote kujielekeza kwenye hoja badala ya mtu binafsi.
Hatua ya Spika Dr Tulia kuagiza kufuta kauli hiyo imekuja baada ya Utaratibu uliombwa na Dr Mwigulu wakati Mbunge wa Tandahimba, Katani Katani akitoa mchango wake Feb 7 2023 baada ya kusema “kuna mambo unapaswa umwambie mtu mdogo sana Mwigulu kaka yangu na rafiki yangu umetutukana wabunge sana, mimi nakuambia unapaswa ukae na utafakari utakapokaa hapa hakuna anayeweza kujadili waganga wa kienyeji, haya tunayojadili ni maisha ya Watanzania”
Kauli hiyo ya Katani ilimuibua Waziri wa Fedha kuomba utaratibu kwa Naibu Spika aliyekuwa akiongoza kikao hicho na baada ya kuzipitia taarifa rasmi leo February 9, 2023 Spika Dr. Tulia amesimama na kusema kuwa wametambua kwamba chimbuko la kauli ya Mbunge Katani na baadhi ya wabunge wengine ambazo wamekuwa wakizitoa bungeni zimetokana na kauli ya Waziri Mwigulu Nchemba kusema ”ebu tujadili mambo mengine huko yanayohusu uganga wa kienyeji na vitu vingine, kwenye hili la uchumi this is my professional”.