Serikali kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imeongeza uwekezaji ambao unatarajiwa kuongeza nguvu ya kudhibiti taarifa ambazo zinamomonyoa maadili ya nchi kama vile picha za ngono.
Kauli hiyo imetolewa Bungeni Dodoma leo February 10, 2023 na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknoloji ya Habari, Nape Nnauye wakati akijibu swali la Mbunge wa Kinondoni, Abbas Tarimba aliyeuliza kama Serikali ipo tayari kuchukua hatua za kuzuia picha za ngono kuonekana kwenye simu ili kuokoa Vijana.
Waziri Nape akijibu amesema mfumo unaokuja ukikamilika masuala ya picha za ngono yatakuwa yamedhibitiwa kwa kiasi kikubwa aidha amesema Serikali ina uwezo wa kufuatilia na kujua anayesambaza picha chafu hivyo amewaomba Watanzania endapo Mtu atatumiwa picha chafu ni bora kuifuta.