Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) amewataka Watendaji wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii wasimamie utekelezaji wa programu zinazoelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa Uhifadhi na kutembelea vivutio vya Utalii hapa nchini.
Ameyasema hayo leo alipofanya kikao kazi na watendaji hao katika Chuo cha Taaluma ya Wanyamapori – Pasiansi jijini Mwanza akisisitiza kuwa ni vyema jamii ikaelimishwa juu ya umuhimu wa uhifadhi kuanzia ngazi za vijiji,Kata,Wilaya na Mikoa ili wananchi wawe na uelewa wa pamoja kuhusu tija inayopatikana kupitia uhifadhi jambo litakalorahisisha usimamizi wa maeneo yaliyohifadhiwa .
Aidha, amebainisha kuwa kupitia maamuzi ya kikao hicho taasisi za Wizara zitatangaza utalii kwa kutumia fursa ya kushiriki kwenye matamasha mbalimbali ili kuwajulisha wananchi umuhimu wa kutalii huku akitoa wito kwa Watanzania wawe wazalendo, watembelee vivutio mbalimbali vilivyoko nchini.
“Nawaomba watanzania wote tuwe wazalendo tukatembelee vivutio vyetu vya utalii kwani gharama ni ndogo sana haizidi fedha ya kitanzania shilingi elfu kumi (10), Kutalii kuna faida kama vile kujifunza, kupumzisha akili kwa kutoa msongo wa mawazo pia kuvijua na kuvitambua vivutio mbalimbali vilivyoko hapa nchini”
Kikao hicho kimehudhuriwa na viongozi wa Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori Pasiansi, Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Chuo cha Taifa cha Utalii Kampasi ya Mwanza na Idara ya Utalii.