Watu watano wanashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Manyara kwa makosa ya kukutwa na nyara za Serikali ikiwemo nyama ya Twiga inayokadiriwa kuwa na thamani ya zaidi ya Tsh. Milioni 87 kinyume cha sheria.
RPC wa Manyara George Katabazi amesema mnamo February 14, 2023 huko katika Kijiji cha Minjingu Wilaya ya Babati Mkoa wa Manyara Jeshi hilo kwa kushirikiana na Hifadhi ya Wanyamapori (TAWA) na Afisa Wanyamapori Wilaya ya Babati walimkamata Paul Richard (23) na Masiaya Lais (19) wakiwa na nyama ya Twiga yenye thamani ya Shilingi Milioni 30 huku wakiwa na silaha aina ya Gobole, mkuki pamoja na Sime.
Kamanda Katabazi amesema pia Feb 25,2023 huko katika Hifadhi ya Jamii Makame Wilaya ya Kiteto, Polisi kwa kushirikiana na Askari wa Hifadhi walimkamata Meshaki Mohamed (54) akiwa na nyama ya Twiga yenye thamani ya Shilingi Milioni 30, akiwa ana Gobole, kisu pamoja na unga wa baruti.
Aidha Kamanda Katabazi amesema katika tarehe hiyohiyo katika Kijiji cha Kitwai “B” Wilaya ya Simanjiro walikamatwa Watuhumiwa wawili Nasibu Ali (45), Juma Mussa (28) wote wakiwa Wakazi wa Kilindi, Tanga wakiwa na nyamapori ya mnyama Tandala na Digidigi zenye thamani ya zaidi ya shilingi Milioni 27 wakiwa wanatumia usafiri wa pikipiki, huku Jeshi la Polisi likitoa wito kwa Wananchi kuacha kujihusisha na Biashara ya nyara za Serikali.