TikTok ilitangaza mapema hii leo kwamba kila akaunti ya mtumiaji aliye na umri wa chini ya miaka 18 atakuwa na chaguo la kikomo cha muda wa kutumia application hiyo, ambapo kila kijana aliye na umri chini ya miaka 18 matumizi ya mtandao huo utakuwa ni wa lisaa limoja tu kwa siku, ikiwa ni moja ya hatua kali zaidi za kampuni hiyo ya mitandao ya kijamii kuzuia vijana kutumia muda mwingi kwenye simu zao.
Ingawa watumiaji wa TikTok wenye umri chini ya miaka 18 watakuwa na uwezo wa kuzima mpango huo mpya ambao utaanza kutumika katika wiki kadhaa zijazo tiktok inatumai kwamba mabadiliko hayo yanaweza kuimarisha ustawi wa kidijitali wa watumiaji wenye umri mdogo kwa kuwahitaji kuchagua kuweka vikomo vya muda wa kutumia kifaa, badala ya kutumia muda mwingi kutumia mtandao huo.
Ikiwa kikomo cha dakika 60 kimefikiwa, watumiaji wataombwa waweke nambari ya siri inayowahitaji kufanya uamuzi wa kuongeza muda watakaotumia kupitia video mbali mbali kwenye application hiyo.
Hatua hiyo imekuja baada ya TikTok na majukwaa mengine ya mitandao ya kijamii kukabiliwa na uchunguzi wa miaka mingi juu ya athari zao kwa watumiaji wenye umri mdogo, TikTok pia inakabiliwa na shinikizo kubwa kutoka serikali ya Marekani juu ya wasiwasi wa usalama kutokana na uhusiano na serikali ya China kupitia kampuni mama ya Bytedance pamoja na mjadala mpya wa uwezekano wa Marekani kupiga marufuku programu ya video ya muda mfupi.
Tiktok pia ilitangaza ujio wa kipengele kitakacho wawezesha wazazi kuuunganishwa na akaunti za watoto au vijana wao na kuweka vidhibiti. Wazazi wataweza kuchuja video zenye maneno au maudhui ambayo hawataki zionekane kwenye page zao, kuweka kikomo maalum cha muda wa kutumia application hiyo kwa siku na kuweka ratiba maalum ya kudhibiti upokeaji wa taarifa za TikTok. Mitandao mengine ikiwa ni pamoja na Instagram na Snapchat vile vile imetoa vidhibiti vya ziada vya wazazi na vipengele vinavyohimiza vijana kuchukua mapumziko ya kutumia vifaa vyao.