Rais wa Kenya William Ruto na kiongozi wa Upinzani Raila Odinga wameungana katika ukosoaji wao wa uamuzi wa mahakama ya juu zaidi wa wiki iliyopita ambao unaoruhusu jumuiya ya wapenzi wa jinsia moja kusajili Vikundi vya harakati zao nchini Kenya.
Ijumaa iliyopita Mahakama ya Juu iliamua kwamba uamuzi wa bodi ya asasi zisizo za serikali nchini Kenya kukataa kuandikishwa kwa jumuiya ya wapenzi wa jinsia moja au kikundi kingine chochote chenye maneno ‘mapenzi ya jinsia ndani yake, ulikuwa kinyume cha sheria.
Mahakama ilisema kuwa kunyima kundi hilo kusajiliwa kwa misingi ya jinsia zao ni ukiukaji wa haki zao za kikatiba za kujumuika na uhuru wa kutobaguliwa.
Katiba ya Kenya inaruhusu ndoa kati ya watu wa jinsia tofauti pekee, huku kanuni ya adhabu inaadhibu ngono ‘kinyume na utaratibu wa asili’ kwa kifungo cha hadi miaka 14 jela.
Tofauti na Rais pia Kiongozi wa Upinzani Raila Odinga amenukuliwa akisema kuwa haikuwa jukumu la idara ya mahakama kutunga sheria.
Hivi karibuni kumekuwa na ukosoaji dhidi ya wapenzi wa jinsia moja nchini Kenya na kanda nzima ya Afrika mashariki.