Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limeendesha kampeni ya kutunza mazingira kwa kupanda miche ya miti katika Wilaya ya Kilolo, mkoani Iringa.
Kampeni hii iliyoanza tokea tarehe 1 Machi 2023 inakwenda sambamba na wiki ya Kimataifa ya Wanawake Duniani itakayofikia kilele chake mnamo tarehe 8 Machi 2023.
TANESCO kwa kushirikiana na Jukwaa la Wanawake ambapo walipanda miche 500 aina ya mivengi ambayo ni maarufu kwa kuhifadhi maji kwa muda mrefu pembezoni mwa mto Mtitu uliopo katika Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa unaopelekea maji yake katika mto Rufiji ambao utatumika kufua umeme kupitia mradi wa kimkakati wa bwawa la Julius Nyerere (JNHPP).
Lengo la kampeni hii ni kutunza mazingira pamoja na kulinda vyanzo vya maji vinavyotiririsha maji yake katika mabwawa yetu ya kufua umeme.
Kampeni hiyo ilizinduliwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo, Mhe. Anna Msola na kupongeza jitihada zilizofanywa na TANESCO katika kuhakikisha inalinda vyanzo vya maji.
Amesema mito mingi iliyoko Wilayani Kilolo mkoani Iringa inatiririsha maji yake kwenye mto Ruaha Mkuu ambao ndio chanzo kikubwa kinachopeleka maji kwenye bwawa la Julius Nyerere (JNHPP).
”Wananchi tunawaomba muwe mabalozi wazuri katika utunzaji wa miti hii kwani ndio hazina kubwa kwenye vyanzo vyetu vya maji ambayo yanatumika pia kwenye matumizi ya nyumbani” alisema Mhe. Msolla.
Awali akizungumza kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi, Meneja wa Wilaya ya Kilolo TANESCO, Mhandisi Mwamvita Ally amesema kuwa kampeni hii ya Panda miti, mvua ndii, umeme ndindindii ina lengo la kupanda miti kwenye maeneo yote ya vyanzo vya maji na kuwataka wananchi kuhakikisha wanaitumza kwa kishirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo.
Kwa upende wake Meneja Mawasiliano na Uhusiano kwa wadau, Elihuruma Ngowi amesema mabwawa ya kufua umeme kama ya Mtera, Kihansi, Kidatu, Nyumba ya Mungu, Hale na Pangani yanategemea sana vyanzo vya maji vya uhakika ili yaweze kufua umeme wa uhakika muda wote.
Amesema mradi wa bwawa la kufua umeme la Julius nyerere (JNHPP) ambao ujenzi wake umefikia asilimia 83.3 unategemea sana vyanzo vya maji vinavyotititisha maji yake kwenye mto Ruaha Mkuu pamoja na vyanzo vya mito mingine kama mto Ruwegu na mto Kilombero na kuleta maji mto Rufiji ili yatumike kufua umeme, ikolojia, kilimo, uvuvi na huduma za maji safi na salama.
Naye Mwenyekiti wa Jukwaa la Wanawake wa Kanda ya Mashariki TANESCO, Prisca Maziwa amelishukuru Shirika kuwaruhusu wanawake kuendesha kampeni hii kwani ni miongoni mwa vipaumbele vya Shirika kutunza mazingira hususani kwenye maeneo ya vyanzo vya maji ili kuepusha ukame ambao huliathiri Shirika katika ufuaji wa umeme pindi ukame unapolikumba Taifa letu.
Aidha, TANESCO ilikabidhi miche ya miti ya mivengi iliyobakia kwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo kwa ajili ya kwenda kuipanda kwenye vyanzo vingine vya maji ili kuendelea kutunza na kuhifadhi mazingira hasa kwenye maeneo ya vyanzo vya maji.