Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imewakumbusha Wananchi kwa ujumla na Waagizaji wa mizigo kutoka nje ya chi kupitia utaratibu wa kuchangia Makasha (Containers) ujulikanao kama “Cargo consolidation & De-consolidation” kwa kutumia Mawakala wanaofanya shughuli hizi, juu ya umuhimu wa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu zinazosimamia utaratibu huo kama zilivyoainishwa.
“Ni takwa la kisheria kwa Mwagizaji wa mizigo anayetumia utaratibu huu kuhakikisha Wakala atakayemtumia kusafirisha mzigo wake ana leseni hai ya uendeshaji wa shughuli za Cargo inayotolewa na Shirika la Wakala wa Meli Tanzania (TASAC) kabla ya kuanza kufanya nae biashara”
“Anatumia Wakala wa Forodha mwenye leseni hai inayotolewa na TRA kupitia kwa Kamishna wa Forodha na Ushuru wa Bidhaa, Wakala wa Usafirishaji anatoa nyaraka za kusafirisha mizigo kwa kila Mchangiaji kwenye Kasha husika, nyaraka hizi ndizo zitakazotumika kugomboa mizigo ya kila Mchangiaji”
“Anapata risiti sahihi ya huduma ya kusafirisha mizigo (EFD) kutoka kwa Wakala wa Usafirishaji pamoja na risiti ya huduma ya kugomboa mizigo bandarini ambayo inatolewa na Wakala wa Forodha”