Mlipuko wa virusi vya Marburg nchini Equatorial Guinea umesababisha vifo vya watu 20 katika kipindi cha miezi miwili iliyopita, Shirika la Afya Duniani limesema Alhamisi.
Mlipuko wa homa ya kuvuja damu, ambayo inafanana na ugonjwa hatari wa Ebola, sasa umeenea na kuvuka jimbo la Kie-Ntem, ambako ulisababisha vifo vya kwanza kujulikana mwezi Januari.
Ugonjwa huo wa virusi hivyo vya Marburg umefika Bata ambao ni mji mkuu wa kibiashara wa taifa hilo.
WHO imesema kuwa “hadi sasa, kuna uwezekano wa visa 20 na vifo 20” nchini humo.
Visa hivyo vipya vimeripotiwa kutoka katika maeneo ya Kie-Ntem upande wa mashariki na katika majimbo ya Litoral kwa upande wa magharibi na Centro Sur, ambayo yote yanapakana na nchi za Cameroon na Gabon.
Mkurugenzi wa shirika la afya duniani, WHO kanda ya Afrika, Dr Matshidiso Moeti, amesema mlipuko wa virusi vya Marburg, ni ishara tosha kwamba nchi zinatakiwa kuongeza kasi ya kudhibiti maambukizo zaidi, ili kuepusha ugonjwa huo kuenea kwenye maeneo mengi.