Nchini Kenya, muungano wa upinzani wa Azimio la Umoja, umeitisha tena maandamano mapya leo jijini Nairobi kulalamikia kupanda kwa gharama ya maisha na kudai kile wanachosema ni ushindi wao wa kisiasa baada ya uchaguzi wa maka uliopita licha ya katizo la maandamano ya wiki iliyopita.
Maandamano ya Jumatatu iliyopita, nchini Kenya yalisambaratisha shughuli za kiuchumi jijini Nairobi, na kusababisha pia kifo cha Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Maseno, Magharibi mwa nchi hiyo.
Wito umekuwa ukitolewa kwa viongozi hao wawili, Rais Ruto na Odinga kuketi pamoja na kutafuta suluhu kama njia moja ya kuliepusha taifa hilo kutumbukia katika mzozo wa kisiasa.
Licha ya wito huo kutoka kwa mashirika ya kiraia na viongozi wa kidini katika taifa hilo la Afrika mashariki, Odinga na Ruto wameonekana kupuuza wito huo na kuendelea na msimamo yao mikali ya kisaisa.
Maandamano ya wiki yanafanyika wakati huu rais William Ruto akiwa nje ya nchi kwa ziara ya siku nne katika mataifa ya Ujerumani na Ubelgiji.
Hata hivyo, jeshi la Polisi, limeharamisha maandamano hayo. Japhet Koome ni Inspekta Jenerali wa polisi nchini humo.
“Mimi kama inspekta generali wa polisi hakuna maandamano nimeruhusu, hayo ni mambo ya kisiasa na yanafaa kusuluhishwa kisiasa.”amesisitiza Japeth Koome.
Lakini mpaka sasa kiongozi huyo waupinzani Raila Odinga, bado amewasisituza kwa kuwaambia wafuasi wake wajitokeze kwa wingi na kusisitiza kuwa maandamano hayo ni ya amani, akiwa na ujumbe kwa jenerali wa polisi;
“Hayo maandamano tunafanya ni ya amani na sheria inakubali”