Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Mkoani Tanga, Jokate Mwegelo yupo kwenye ziara Nchini Afrika Kusini yenye lengo la kutangaza zao la mkonge na mambo ya uhifadhi wa Wanyamapori na mazingira ambapo akiwa huko amezungumzia umuhimu wa ushiriki wa Vijana katika ujenzi wa Bara la Afrika.
DC Jokate amesema atatumia fursa hiyo kutangaza chapa ya ‘Made In Korogwe’, ikiwa ni sehemu ya kutangaza bidhaa zinazozalishwa Korogwe pamoja na kutangaza kazi za Wajasiriamali Wanawake na Vijana wa Kitanzania, pia kujadili jinsi Wajasiriamali wa Afrika Kusini na Tanzania wanavyoweza kushirikiana kukuza ukuaji na maendeleo Afrika “Nina furaha kutembelea Afrika Kusini na kuungana na Wafanyabiashara na Viongozi, maono yangu ni kujenga Bara bora la Afrika”
Jokate ametembelea Ubalozi wa Tanzania ili kujadili ushirikiano na Maj.Gen (Mstaafu) Gaudence Milanzi, Balozi wa Tanzania Nchini Afrika Kusini na Wafanyakazi wa Ubalozi, pia ataandaa chakula cha jioni na baadhi ya Watu muhimu Afrika Kusini ili kujadili jinsi Wajasiriamali nchini Afrika Kusini na Tanzania wanaweza kufanya kazi pamoja ili kukuza ukuaji na maendeleo Afrika.
Pia ametembelea maduka ya Wanawake Wajasiriamali Afrika Kusini ili kuona jinsi wanavyoweza kupanua kazi na biashara zao hadi Korogwe na pia kujadili jinsi Wajasiriamali wa Tanga wanaweza kuuza bidhaa zao nchini Afrika Kusini.