Wafanyabiashara wadogo wadogo maarufu kama ‘Machinga’ katika soko la Tegeta Nyuki Dar es Salaam wamesema kwamba suala la usafi katika masoko bado ni tatizo hasa kutokana na ukosefu wa vifaa mbalimbali kwa kuzolea taka.
Hayo yamebainishwa na Weche Moshi ambaye ni Katibu wa Soko hilo baada ya kufanya usafi kwa kushirikiana na Wadau wa Mazingira ambao pia wamewakabidhi vifaa vya usafi vyenye thamani ya Shilingi Milioni Tano.
“Soko la Tegeta Nyuki lipo mbali na City Center lakini huwezi kuamini wadau wametutembelea, lakini tunashukuru vifaa vyote vya usafi tumeachiwa na tutavitumia kama uongozi wa soko,”.
“Suala la usafi kwenye masoko bado ni tatio lakini kama mlivyoona nyie ni mashuhuda tumefanya kazi kubwa na hii kazi tutaendelea kuienzi, tunaenda kutengeneza utayari na utaratibu wa usafi kwa kila maeneo ili kuepukana na mlundikano wa takataka za muda mrefu,”amesema Katibu.
Kwa Upande wake, mdau wa Sekta ya Mazingira, Denis Kato amesema—“Nikiwa kama mdau wa mazingira, napenda mazingira masafi napenda mazingira kwa sababu ni uhai na bila kuwa na mazingira mazuri katika maeneo mbalimbali biashara hazitawezekana,”.
“Kwa siku ya leo tukasema turudi kwa wale tunaowahudumia kwa ajili ya kutengeneza mazingira masafi katika maeneo yao ya biashara, kama hapa tupo katika soko la Tegeta Nyuki kuna Wajasiriamali mbalimbali ambao kimsimgi tunawahudumia, tukasema tuje tuungane nao na kuwahamasisha kufanya usafi tukiwa kama wadau wa mazingira,” amesema Kato.