Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa imekutana katika kikao chake cha kawaida leo Jumamosi, Aprili 1, 2023, chini ya Mwenyekiti wa CCM, ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu ambapo imepokea na kujadili kwa kina masuala mbalimbali ya kitaifa, ikiwemo Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Taarifa ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), kwa mwaka wa fedha 2021/22
Halikadhalika, imetoa maelekezo kwa Serikali kuwafuatilia watu wote wanaotumia dhamana za uongozi vibaya na kushindwa kuweka maslahi ya nchi na uzalendo mbele katika nafasi walizoaminiwa kutumikia watu, badala yake wanaweka maslahi binafsi.
“Kamati Kuu imesikitishwa na kuwepo baadhi ya maeneo mengine ambayo bado yanatakiwa kufanyiwa kazi ili kuondoa mapungufu/udhaifu uliobainishwa, ikiwa ni pamoja na mifumo ya malipo na ukusanyaji wa mapato kutokusomana, kuwepo kwa baadhi ya watumishi wa umma wasiokuwa waadilifu, hali inayosababisha serikali kukosa mapato na kupata hasara, uwepo wa mashirika ya umma yanayojiendesha kwa hasara na vitendo vya ubadhirifu wa mali na rasilimali za umma, kama vile kuongeza bei za manunuzi ya Serikali”