Baadhi ya waandamanaji wamekusanyika nje ya kiwanda cha kuzalisha silaha cha Israel mjini Leicester, ambapo sanjari na kulaani jinai za kikatili za Israel dhidi ya Wapalestina, lakini wametaka kufungwa haraka kwa kampuni hiyo.
Waandamanaji hao wametoa onyo ya siku 30 ya kufungwa kwa kampuni hiyo, na iwapo haitafungwa muhula huo utakapomalizika, basi watachukua kile walichokiita ‘hatua ya umma.’
Maandamano kama hayo yameshuhudiwa pia katika miji ya Glasgow na Brighton, ambapo waandamanaji waliokuwa wamebeba bendera ya Palestina, walikuwa na mabango pia yenye orodha ya jinai zinazofanywa na Wazayuni dhidi ya wananchi madhulumu wa Palestina.
Kampuni hiyo ya Kizayuni mjini Leicester ya UAV Tactical Systems inamilikiwa na shirika kubwa la kuzalisha silaha la utawala haramu wa Israel la Elbit Systems.
Harakati ya ‘Palestine Action’ inasema silaha hizo zinazozalishwa nchini Uingereza na kampuni ya Israel si tu zinatumika dhidi ya Wapalestina, lakini zinatumika pia kuwaua, kuwakandamiza na kudhumu watu wengine katika maeneo mbalimbali ya dunia.