Rais wa Tunisia, Kais Saied amejitokeza na kukanusha madai kuwa hali yake ya afya inadhoofika, baada ya kutoonekana hadharani kwa kipindi cha wiki mbili.
Kupitia mkanda wa video uliowekwa kwenye ukurasa wa Facebook, kiongozi huyo wa Tunisia, amesema ripoti hizo ni za kupotosha na hazipaswi kuaminiwa.
Amewashtumu wapinzani wake wa kisiasa kwa kueneza taarifa za uongo na kuongeza kuwa watu hao wanapaswa kuchukuliwa hatua za kisheria.
Aidha, Saied mwenye umri wa miaka 65, amewashtumu wapinzani wake kwa kujaribu kutengeneza mzozo ili ionekana kuwa kuna fursa ya wao kuingia madarakani.
Kabla hajajitokeza, upinzani ukiongozwa na kiongozi wa muungano wa National Salvation Front, Ahmed Nejib Chebbi ulikuwa umetoa taarifa kwa serikali kujitokeza na kueleza aliko rais Saied, baada ya kudai kuwa alikuwa anaumwa na hali yake ilikuwa mbaya.
Wapinzani nchini Tunisia wamekuwa wakimtaja kiongozi huyo kama dikteta baada ya kulivunja bunge na serikali mwezi Julai mwaka 2021 na baadaye kuifanyia marekebisho Katiba ili kujipa nguvu zaidi.