Benki ya Azania katika jitihada zake za kumkomboa Mwanamke kiuchumi, imezindua akaunti yenye kutoa mikopo yenye riba ya asilimia 1 tu kwa mwezi. Akaunti hiyo ambayo itawakomboa na kuwaongezea mitaji Wanawake na kuwawezesha kujiinua kiuchumi inajulikana kwa jina la Akaunti ya Mwanamke-Hodari inayofunguliwa Bure na haihitaji kima cha chini cha kuendeshea Akaunti hivyo mwenye akaunti ataweza kutoa Fedha zake bila kikomo na bila makato.
Hafla ya uzinduzi wa Akaunti hiyo imefanyika katika Hoteli ya Hyatt Regency jijini Dsm, mgeni rasmi katika shughuli hiyo alikuwa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na wenye Mahitaji Maalum Mh. Dorothy Gwajima.
Akaunti hiyo imezinduliwa ikiwa ni muendelezo wa mkakati wa Benki hiyo katika kuwainua kibiashara Wanawake sambamba na kuunga mkono jitihada za Serikali ya Dk. Samia Suluhu Hassan katika kuwawezesha Wanawake kiuchumi.
Akizungumza katika uzinduzi wa Mikopo hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo Bi. Esther Mang’enya alisema kuwa Akaunti hii yenye mikopo nafuu ni mahususi kwa ajili ya Wanawake ambao mara nyingi katika masuala ya mikopo huwa wanashindwa kukidhi vigezo na masharti ya kukopesheka.
Kupitia Akaunti hii ya Mwanamke-Hodari, mkopaji atajipatia mkopo wenye masharti nafuu sana ikiwemo Riba ya 1% tu, pia endapo mkopaji atapoteza maisha au kupata maradhi yatakayofanya ashindwe kuendelea kulipa mkopo wake mkopo huo utalipwa na Bima, vilevile mkopaji ataweza kukopa kiwango hadi kufikia mara nne ya kiasi kilichopo kwenye akaunti yake. Kuhusu Dhamana, kupitia utaratibu uliowekwa na Benki hiyo na wadau wake, mkopaji ataweka dhamana yenye thamani ya Asilimia 25% tu na si asilimia 100% kama ilivyo kwenye mikopo ya kawaida.
Naye Mgeni rasmi katika hafla hiyo, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na wenye Mahitaji Maalum Mh. Dk.Dorothy Gwajima aliipongeza menejimenti ya Benki ya Azania kwa kubuni huduma hii ambayo inawagusa Wanawake moja kwa moja.
Mbali na kuipongeza pia Mh. Gwajima aliwasihi Wanawake nchini kuchangamkia Akaunti hii ili waweze kujiwekea akiba bila masharti na kunufaika na Mikopo yenye masharti rahisi kama hii.
‘Mmefanya jambo kubwa leo na kuhakikisha Benki ya Azania inamkomboa Mwanamke. Benki ya Azania ni muongo mwa benki zinatoa kipeumbele kwa wanawake. kufanya juhudu za kutoa elimu ya kifedha kwa wanawake kwani wanawake wengi hawana elimu ya kifedha, na matatizo mengi katika ndoa chanzo ni uchumi” Gwajima