MIAKA mitano iliyopita, ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ilizua mjadala mkubwa kitaifa baada ya kuibuka kwa hoja ya kutojulikana ziliko shilingi trilioni 1.5 zilizotengwa kwenye bajeti ya mwaka 2016/2017.
Aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Mjini wakati huo kupitia Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, ndiye aliyehoji zilipo fedha hizo kutokana na ukweli kwamba hesabu za Mfuko Mkuu wa Serikali zilionyesha makusanyo yalikuwa shilingi trilioni 25.3, lakini matumizi yakawa kiasi cha shilingi trilioni 23.79. Hiyo ndiyo ilikuwa ripoti ya kwanza ya aliyekuwa CAG, Profesa Mussa Assad, kwenye utawala wa hayati John Magufuli.
Mijadala iliyofuata ripoti ndiyo inaelezwa kuanza kwa uhusiano mbovu baina ya Bunge, Rais Magufuli na Assad mwenyewe – kiasi kwamba ilibidi CAG huyo baadaye aondolewe kwenye wadhifa wake huo.
Serikali, kupitia kwa aliyekuwa Naibu Waziri wa Fedha, Dk. Ashatu Kijaji, ilitoa majibu Bungeni na kueleza kuwa mkanganyiko uliojitokeza ulitokana na kuanza kwa matumizi ya mfumo wa IPSAS Accrual. Mfumo wa IPSAS Accrual ni mfumo wa kihasibu ambapo mapato hutambuliwa baada ya muamala kukamilika na si wakati fedha inapopokewa na matumizi, hutambuliwa pale tu muamala unapokamilika na si wakati pesa inapolipwa.
Kwa wanaokumbuka, huu ndiyo wakati pia aliyekuwa Katibu Mwenezi wa CCM, Humphrey Polepole, alipofanya mkutano na waandishi wa habari akitumia chati ili kujaribu kutoa ufafanuzi.
Hata hivyo, maelezo ya serikali hayakufua dafu wakati huo kwa sababu zilikuwepo hoja nyingine kutoka kwa wataalamu zilizoonyesha lilikuwepo tatizo la mapato kutowiana na matumizi kihasibu katika hesabu za serikali hata kabla ya IPSAS Accrual.
Kwa mfano, aliyewahi kuwa Mbunge wa Ukonga na mtaalamu wa masuala ya ununuzi na uhasibu, Dk. Milton Mahanga, aliarifu kwamba katika bajeti ya mwaka 2015/2016 – kabla hata ya matumizi ya IPSAS Accrual, kiasi cha shilingi trilioni 1.088 pia hakikujulikana kilipo. Mapato yalikuwa shilingi trilioni 21.109 lakini matumizi yakawa shilingi trilioni 20.021.
Hoja ya Mahanga ilikuwa kwamba kama tatizo hilo lilitokana na IPSAS, halikutakiwa kuwepo kabla yake. Lakini kuwepo kwake kulimaanisha kulikuwa na tatizo la usimamizi wa mapato na matumizi ya fedha za serikali.
Katika ripoti ya CAG ya mwaka 2021/2022 iliyowasilishwa bungeni wiki iliyopita, tatizo la kuwapo kwa pesa ambazo matumizi yake hayajulikani halipo na limeondoka kabisa chini ya utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan. Ushahidi uko wapi?
Upekee wa bajeti ya mwaka 2021/2022
Vitu vichache vya kipekee vinajionyesha katika bajeti ya Tanzania iliyofanyiwa ukaguzi na CAG.
Kwa mfano, kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania kwenye miaka ya hivi karibuni, mapato yaliyopatikana yalizidi makadirio ya bajeti.
Kwenye vitabu vyake, CAG ameonesha kwamba ingawa serikali ilipanga kukusanya kiasi cha shilingi trilioni 36.681 lakini ikakusanya shilingi trilioni 37.992 – ongezeko la asilimia nne kulinganisha na matarajio.
Katika hali ya kawaida, kutokana na ukosefu wa usimamizi uliojionyesha huko nyuma, ongezeko hili la mapato lingezua changamoto na huenda lingepotea.
Lakini kilichotokea ni tofauti. Fedha zote zilizokusanywa na serikali zimepelekwa kwenye Mfuko Mkuu (Consolidated Fund) na kiasi kilekile kilichokusanywa ndicho hicho kimekwenda Serikalini.
Kwa mfano, jedwali la CAG linaonesha kwamba jumla ya makusanyo yote yaliyoingia katika Mfuko Mkuu hadi Juni 30, 2022 yalifikia kiasi cha shilingi trilioni 35.486, lakini matumizi yalikuwa shilingi trilioni 36.063. Itaonekana hapo kwamba matumizi ni makubwa kuliko makusanyo.
Ripoti ya CAG imefafanua kwamba nakisi iliyopo hapo, kiasi cha shilingi bilioni 577, inatokana na miradi ambayo wafadhili waliamua fedha zitumike kwenye miradi moja kwa moja au ziingie kwenye akaunti za mashirika yanayojihusisha na mambo yaliyofadhiliwa. Hizo ni pesa ambazo hazikuingia kwenye mfuko mkuu wa Serikali.
Hii ni mara ya kwanza katika historia ya karibuni ya Tanzania – hasa baada ya tukio la “trilioni 1.5” ambapo CAG aliruhusiwa kufanya ukaguzi kwenye Mfuko wa Hazina.
Na ukaguzi huo sasa umefichua kwamba lile ‘shimo’ lililokuwepo zamani la kutowiana kwa mapato na matumizi ya serikali, sasa limezibwa.
Matokeo ya hatua hii ni kwamba leo mjadala hauhusu tena wapi zilipo shilingi trilioni kadhaa ambazo zilikusanywa lakini hazijulikani zilipo – mjadala unahusu kilichokusanywa kimetumika vipi.
Mjadala sasa unajikita kwenye namna ambavyo mapato yametumika, siyo kwenye mapato yaliyoyekuka kusikojulikana kwa kutoonekana kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali na kutoidhinishwa na Bunge.
Hii ni hatua kubwa kwa Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan ambaye ndiyo kwanza ametimiza miaka miwili ofisini. Kama wasemavyo Waswahili, yajayo yanafurahisha.