Shirikisho la wachimba Madini nchini Tanzania (FEMATA) kupitia waandishi wa habari hii leo April 15, limetoa taarifa ya kusogezwa mbele kwa tarehe za Tamasha la wiki ya madini Tanzania 2023.
Lengo kuu la kusogeza mbele tarehe hizi ni kutokana na muingiliano wa mpangilio wa shughuli mbalimbali zikiwemo za wiki ya madini Tanzania kuingiliana na sikukuu ya Eid El Fitr,sikukuu ya Muungano na Wizara ya madini kuwasilisha bajeti bungeni hivyo kungeathiri baadhi ya mipango iliyopangwa kwenye sherehe hizo.
Tamasha hilo awali lilipangwa kufanyika tarehe 21 hadi 28 aprili likiwa na lengo la kuwakutanisha wadau mbalimbali wakiwemo wachimba madini wadogo kwa wakubwa, Viongozi wa idara,Mashirika ya maendeleo,asasi za kiraia, wasomi,watoa huduma Migodini, Wataalamu wa Sera za Umma pamoja na wataaluma wa tasnia ya Madini litafanyika tena mwezi mei tarehe 3 hadi 9 mwaka huu.
FEMATA,wamesema kuwa kusogezwa mbele kwa tarehe za tamasha hilo hakutaathiri mipango na taratibu nyingine ikiwa ni pamoja na maonesho ya kazi,makongamano,warsha,semina ,huduma na bidhaa za wadau ,kliniki za madini pamoja na mkutano mkuu wa wanachama wa FEMATA na Gala ya usiku wa madini.
Aidha FEMATA kupita Rais wa chama hicho kimeomba radhi kwa wadau wote na washiriki wa Wiki ya madini Tanzania 2023 pamoja na kuendelea kuiunga mkono na kutoa ushirikiano mpaka pale shughuli hii itakapofanyika.
“Tunaomba wadau wote kutumia fursa hii kuendelea kujiandikisha ili kushiriki Wiki ya madini Tanzania 2023 kupitia tovuti ya FEMATA”John Bina Rais wa FEMATA.