Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) imesema katika hali inayozidi kuwa mbaya, mapigano yanayoendelea kote nchini Sudan yanazuia sana operesheni za kibinadamu.
Stephane Dujarric, msemaji mkuu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, alisema kwenye mkutano na waandishi wa habari kwamba wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu walikuwa wamefungiwa mjini Khartoum, na kutakiwa kukaa katika nyumba zao au nyumba za marafiki, majirani au wafanyakazi wenzao
OCHA imesema kuna uwezo mdogo wa kuhamisha wafanyakazi na vifaa, na kuongeza kuwa kushambulia mali na vifaa vya kibinadamu kutaathiri pakubwa uwezo wake wa kuanza tena shughuli za kuokoa maisha.
OCHA pia imesema Shirika la Mpango wa Chakula Duniani WFP lilisimamisha kwa muda shughuli kufuatia mauaji ya wafanyikazi wake watatu kwenye mapigano huko Darfur Kaskazini.
Mashambulizi dhidi ya vituo muhimu vya umma, ikiwa ni pamoja na afya, maji na usafi wa mazingira huathiri sana upatikanaji wa huduma muhimu.