Maafisa wa usalama Kenya wamefukua miili 47 hadi kufikia Jumapili kwenye shamba linalomilikiwa na mchungaji wa kanisa moja lenye utata katika kaunti ya Kilifi eneo la pwani ya Kenya huku tayari mhubiri mkuu mwenye misimamo mikali wa Kanisa hilo aliyetambuliwa kama Paul Makenzie Nthenge amekamatwa kwa kuwaamuru wafuasi wake kufunga hadi kufa.
Mkuu wa polisi katika wilaya ndogo ya Malindi, John Kemboi, amewaambia waandishi habari kwamba bado makaburi mengine katika eneo la mchungaji huyo anayehusishwa na imani ya kishirikina hayajafukuliwa.
Watu wanne zaidi walikufa baada ya kugundulika wakiwa wana njaa kali katika kanisa la Good News International linalomilikiwa na mhubiri huyo.
Mchungaji huyo aliwahi kukamatwa mara mbili hapo awali, 2019 na Machi mwaka huu kuhusiana na vifo vya watoto. Kila wakati aliachiliwa kwa dhamana wakati kesi dhidi yake zikiwa zinaendelea mahakamani
Oparesheni ya kufukua makaburi hayo ya siri leo inaingia siku ya nne huku Waziri wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki akitaja yaliyojiri katika kanisa hilo kuwa ni uhalifu wa kiwango kikubwa chini ya Sheria ya Kenya na sheria ya kimataifa na amependekeza kuwekwa kwa sheria thabiti za kudhibiti makanisa, misikiti, na masinagogi nchini ili kuzuia matukio kama haya ya utekelezaji wa uhalifu chini ya kisingizio cha uhuru wa kuabudu.
Mashirika ya kutetea haki za kibinadamu sasa yanazilaumu asasi za kiserikali mjini Malindi katika Kaunti ya Kilifi kwa kutomkabili mapema mhubiri huyo dhidi ya kile kinadaiwa ni kueneza injili potovu kwa waumini wake.