Polisi Nchini Kenya wamesema maiti za Waumini wa Kanisa la Good News International Church linaloongozwa na Mchungaji Paul Mackenzie, ambaye anashikiliwa na Polisi kwa madai ya kuwataka Waumini wake kufa njaa ili kufika Mbinguni kwa haraka, zimefikia 73, miili hiyo imegundulika eneo la Kilifi.
Maiti hizo zimefukuliwa kwenye makaburi ya jumuiya yaliyopo msituni, Mkuu wa Upelelezi wa Kaunti ya Kilifi, Mashariki ya Kenya, Charles Kamau amethibitisha idadi hiyo na ameliambia Shirika la Habari la Reuters kwamba Watu wengine watatu wamekamatwa.
Rais wa Kenya, William Ruto amesema Kiongozi huyo wa Jamii hiyo ya kikristo ni Mhalifu na Gaidi mkubwa, Paul Mackenzie alikamatwa takriban wiki mbili zilizopita baada ya fununu juu ya kuwepo kwa makaburi yaliyokuwa na maiti 31 za Wafuasi wake.
Wafuasi wa Kania la Good News International walikuwa wanaishi kwa kujitenga kwenye eneo la ekari 800 za msitu wa Shakahola nchini Kenya, inadaiwa waliagizwa kufunga mpaka kufa ili kuweza kukutana na Yesu, Idara ya upelelezi ya nchini Kenya imesema Watu 33 wameshaokolewa hadi sasa huku Shirika la msalaba mwekundu la nchini Kenya likisema Watu 112 hawajulikani walipo.