Tulishindwa kuzuia vita isitokee nchini Sudan, ni kauli ya katibu mkuu wa umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, aliyoitoa jijini Nairobi wakati huu mapigano zaidi yakiripotiwa licha ya makubaliano ya kusitisha mapigano.
“Hatukutarajia hili lingefanyika kama ilivyo kwa watu wengine, tunaweza kusema kwamba tulishindwa kuzuia mzozo huu lakini sikifikiri kama kitu ambacho tungefanya hatukufanya.” alisema Antonio Guterres katibu mkuu wa umoja wa mataifa.
Kauli yake imekuja wakati ambapo hivi leo, makubaliano ya usitishaji mapigano kwa siku 7 yaliyoratibiwa na Sudan Kusini, yakitarajiwa kuanza kutekelezwa.
Umoja wa mataifa umetaka kupewa hakikisho kutoka kwa majenerali wawili mahasimu nchini Sudan, kuwa msaada wa kibinadaamu unaohitajika mno, unasafirishwa na kuwafikia waathiriwa wa mapigano.
Katibu mkuu wa umoja huo Antonio Guterres akizungumza na waandishi kwa njia ya video, ameonya kuhusu janga la kibinadamu kufuatia vita vinavyoendelea.
Naye mkuu wa tume ya haki za binadamu ya umoja wa Mataifa, Volker Turk, ameonya kuhusu kuendelea kuripotiwa kwa vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu, vinavyotekelezwa na pande zinazohasimiana nchini Sudan, akitoa wito kwa Jumuiya ya kimataifa kuingilia kati kumaliza mzozo unaoendelea kwenye taifa hilo.
Akihutubia kikao cha baraza la usalama la umoja wa Mataifa, Turk, amesema mzozo unaoendelea Sudan, usipodhibitiwa utasababisha madhara makubwa kwa raia.
“Athari za haki ya haki za binadamu kutokana na mapigano yanayoendelea zimekuwa zakutisha na zinaumiza moyo.” Alisema Volker Turk mkuu wa tume ya haki za binadamu ya umoja wa Mataifa.