Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA) imetoa taarifa kuhusu kugeuza kwa Precision Air iliyokuwa inatoka Dar es salaam kwenda Dodoma May 01,2023 ikiwa na Kikosi cha Yanga ambapo imesema taarifa za awali za uchunguzi wa tukio hilo zimeonesha kulikuwa na ukiukwaji wa taratibu za kiuendeshaji.
Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Hamza Johari amesema “Mnamo May 01, 2023, ndege ya Precision Nambari. PW 602, iliondoka Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA ), saa 12:11 jioni kwa safari ya saa moja kuelekea Dodoma ikiwa na abiria 72, ilitarajiwa kutua uwanja wa ndege wa Dodoma saa 01:13 usiku ambao ni muda zaidi ya masaa ya uwanja huo kufanya kazi.
“Uwanja wa ndege wa Dodoma hufungwa saa 12:30 jioni kutokana na changamoto za miundombinu zilizopo kwa sasa”
“Ilipofika majira ya saa 12:48 jioni Rubani wa ndege hiyo alilazimika kugeuza na kurudi uwanja wa ndege wa JNIA baada ya kushauriwa na muongoza ndege wa zamu, taarifa za awali za uchunguzi wa tukio hilo zimeonesha kulikuwa na ukiukwaji wa taratibu za ki uendeshaji”
“Mamlaka inaendelea na uchunguzi wa kina kuangalia kama Kuna uvunjaji wa kanuni za Usafiri wa Anga katika safari hiyo na endapo itabainika, Mamlaka haitosita kuchukuwa hatua stahiki kwa mujibu wa Sheria, Mamlaka inapenda kuuhakikishia umma kuwa uhairishaji wa kutua katika uwanja wa Dodoma ulifanyika kwa mujibu wa taratibu za usafiri wa anga zilizopo na katika muda wote si usalama wa chombo wala wa abiria angani uliokiukwa”