Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR, limesema linapanga kusaidia wakimbizi 860,000 na waliorejea kutoka Sudan na hivyo likishirikiana na wadau wengine, litahitaji dola milioni 445 kusaidia wakimbizi hao kuanzia sasa hadi mwezi Oktoba mwaka huu.
Kadirio hilo limewekwa kwenye muhtasari wa awali wa mpango wa kikanda wa hatua kwa wakimbizi wa Sudan, ambao umewasilishwa kwa wafadhili. Kimsingi fedha hizo zitashughulikia uungwaji mkono wa haraka wa msaada kwa wakimbizi nchini Chad, Sudan Kusini, Misri, Ethiopia na Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR).
Mpango huo umeundwa na washirika 134 wakiwemo mashirika ya Umoja wa Mataifa, mashirika yasiyo ya kiserikali au NGOs za kitaifa na kimataifa na mashirika ya kiraia.
“Hali ya kibinadamu ndani na nje ya Sudan ni ya kusikitisha kuna uhaba wa chakula, maji na mafuta, upatikanaji mdogo wa usafiri, mawasiliano na umeme, na kupanda kwa bei ya bidhaa muhimu,” amesema Raouf Mazou, kamishna mkuu msaidizi wa operesheni wa UNHCR
Ameongeza kuwa “UNHCR na washirika wana timu za dharura zilizopo na wanasaidia mamlaka kwa msaada wa kiufundi, kusajili wanaofika, kufanya ufuatiliaji wa ulinzi na kuimarisha mapokezi ili kuhakikisha mahitaji ya haraka yanatimizwa. Huu ni mwanzo tu. Msaada zaidi unahitajika haraka.”
UNHCR imekuwa ikiratibu mipango ya dharura na washirika kwa ajili ya watu wapya wanaowasili wakiwemo wakimbizi, wakimbizi wanaorejea na watu wengine katika nchi jirani.
Zaidi ya watu 110,000 sasa wanakadiriwa kuvuka na kuingia katika mataifa mengine huku usitishaji vita haramu ukishindwa kusitisha mapigano makali kati ya wanajeshi wa jeshi la Sudan na wapinzani wa kijeshi ambao wameuwa mamia na kuwalazimisha zaidi ya 330,000 kutoka kwa makazi yao.
Lakini, katika eneo linalokumbwa na njaa na ambalo tayari lina idadi kubwa ya wakimbizi wenye fedha zilizopungua sana, wafanyakazi wa misaada wanaonya kuna maswali mazito juu ya kile kinachowangoja wakimbizi hao wapya mara watakapovuka mpaka.