Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi ametoa wito kwa vijana kuzitumia fursa za kuwepo vyuo vya mafunzo ya amali na ufundi wa fani mbalimbali zikiwemo zinazohusiana na Uchumi wa Buluu ili wajipatie ujuzi utakaowawezesha kupata maarifa ya kuweza kujiajiri na sifa za kuajiriwa.
Ameyasema hayo leo katika halfa ya uzinduzi wa Mradi wa kuwajengea uwezo Vijana kujiajiri na kuajirika katika Uchumi wa Buluu(SEBEP) uliofanyika ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip Airport, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Dk.Mwinyi amesema ni fursa muhimu uwepo wa mradi wa SEBEP katika kukabaliana na changamoto za ajira nchini ambapo Benki ya Maendeleo ya Afrika(AFDB) itachangia asilimia 90 ya mradi huu ambao utagharimu dola za Kimarekani Milioni 50 na Serikali itachangia asilimia 10.
Vilevile mradi huo wa SEBEP una lengo la kuwajengea uwezo Vijana na kuwapatia ujuzi unaofaa ili waweze kukabiliana na soko jipya la ajira kwenye sekta ya Uchumi wa Buluu.