Makubaliano ya kikomo cha deni bado hayajakaribia kwa White House huku wabunge wakiondoka katika mji mkuu wa taifa na hatari ya kutolipa malipo kwa mara ya kwanza, bila mswada wa kupigia kura, wabunge wanaondoka ingawa watapewa notisi ya saa 24 ili kurejea ikiwa na wakati makubaliano yatafikiwa.
Rais wa Marekani Joe Biden alisema Alhamisi kwamba mazungumzo na wabunge wa chama cha Republican ya kuongeza kikomo cha kukopa cha serikali ya Marekani, na kuweka viwango vya matumizi ya siku zijazo, yanakwenda vizuri, huku akiwahakikishia Wamarekani kwamba serikali haitakwepa wajibu wake.
Wafanyakazi wa White House ambao hushughulikia masuala ya bajeti, waliendelea na mazungumzo na wawakilishi wa Spika wa baraza la wawakilishi, Mrepublican Kevin McCarthy, katika hatua za mwisho mwisho za kukagua maudhui ya makubaliano hayo,.
Hata hivyo, hakuna makubaliano yoyote yaliyotangazwa wakati wabunge walianza kuondoka Washington, kwelekea wikendi ya sikukuu ya kila mwaka ya kuwakumbuka wanajeshi wa Marekani waliopoteza maisha yao wakati wakilitumikia taifa.
Baraza la Wawakilishi linalodhibitiwa na chama cha Republican halijapangiwa kurejea hadi Jumanne – siku mbili tu kabla ya Juni mosi, tarehe ambayo waziri wa fedha, Janet Yellen, anasema serikali inaweza kukosa pesa, ili kutimiza majukumu yake ikiwa kikomo cha deni la $ 31.4 trilioni hakitaongezwa, ili serikali iweze kukopa pesa zaidi.