Wito umetolewa kwa wafanyabiashara na wawekezaji kutumia bandari ya Tanga ambayo imefanyiwa maboresho makubwa ikiwemo kuongeza kina cha maji kutoka mita 3 hadi 13 pamoja na upanuzi wa magati yote mawili ambayo yameongeza tija na ufanisi katika utoaji huduma ikiwemo mizigo kupakuliwa kwa wakati.
Wito huo umetolewa leo Ijumaa Mei 26, 2023 na Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Hashim Mgandilwa akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake ambapo amesema maboresho katika bandari hiyo yamegharimu takriban shilingi bilioni 429.
Kufuatia maboresho hayo, Mgandilwa amesema yamefanya Wilaya ya Tanga na Mkoa wa Tanga kwa ujumla kuingia katika historia ya utoaji huduma bandarini hapo ikiwa ni pamoja na meli kupaki kwenye gati.
“Tanga tumeingia katika historia ambapo kwa mara kwanza meli kuja kupaki kwenye gati ambapo kwa miaka mingi meli zilikuwa zinapaki ndani ya maji umbali kilometa 1.7” alisema Mgandilwa na kuongeza
“Hata zile gharama ambazo watu walikuwa wanazilalamikia za mipakuo au gharama za kuhudumia shehena mara mbili (double handling) sasa hazipo tena. Ni wakati sasa wafanyabiashara kutumia fursa hii”
Vilevile Mgandilwa, amewasihi Wafanyabiashara kutojihusisha na magendo kwani athari zake ni kubwa lakini pia vyombo vya Ulinzi na Usalama katika kuyadhibiti magendo hayo viko macho.
“Serikali ya awamu sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imetoa boti mpya kwa ajili ya kudhibiti magendo lakini pia vyombo vyetu vya ulinzi na usalama viko macho kuhakikisha kuwa hakuna magendo yanayoingia kupitia lango la wilaya yetu ya Tanga” alisisitiza Mgandilwa
Akielezea kuhusu umuhimu wa kutumia bandari ndogo zilizorasimishwa na suala zima la udhibiti wa magendo, Mkuu huyo wa Wilaya amesema…“Niwaombe Watanzania, tuone umuhimu wa kutumia bandari ambazo ni rasmi , kufanya magendo ni hatari, unaweza ukawa na mtaji wa shilingi milioni 5 au 6 ukifanya magendo na ukakamatwa unapoteza vyote hadi huo mtaji wako. Hakuna ulazima wa kupoteza mtaji wako wakati unaweza kufuata sheria na mambo yakaenda vizuri”
Kwa upande wake Afisa Masoko Mwandamizi wa Bandari ya Tanga, Rose Tandiko amesema, zoezi la urasimishaji wa bandari ndogo za Pangani, Kipumbwi na Mkwaja na Sahare umeleta matokeo chanya katika usimamizi wa bandari katika kuwezesha mazingira ya kufanya biashara kati ya Mkoa wa Tanga na wilaya zake pamoja na maeneo ya visiwani kuwa rahisi, nafuu na yenye kuleta tija
Bi. Tandiko ameongeza kuwa, uwepo wa bandari hizi ndogo umechochea kasi ya ongezeko la mapato katika Mkoa wa Tanga.
“Uwepo wa bandari ndogo zilizorasimishwa umeleta chachu ya kuongezeka kwa mapato katika Mkoa wa Tanga na pia kuwafanya wafanyabiashara kuwa huru katika shughuli zao kwani kabla ya urasimishaji wa bandari hizi zilikuwa zinatambulika kama bandari bubu” alisema Bi. Rose
Naye mmoja wa wakazi katika bandari ndogo ya Sahare, Bwana Bwembe Hassan Idrisa ameeleza kuwa, kurasimishwa kwa bandari hiyo kumechochea ukuaji wa viapto vyao kwani wafanyabiashara wanaoshusha katika bandari hiyo wameongezeka na pia fursa ya ajira hususan kwa vijana kupatikana katika maeneo mbalimbali ikiwemo upakuaji wa mizigo na Uvuvi.
Urasimishaji wa bandari ndogo unatajwa kuwa njia bora ya kukuza mapato ya Serikali kwa kuweka mazingira salama kwa Wananchi kwa ajili ya shughuli za ikiwemo usafirishaji wa mizigo. Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) imepewa majukumu makubwa yanayotokana na sheria ya Bunge iliyoanzisha TPA.
Sheria namba 17 ya mwaka 2004 inayosema kwamba kazi za TPA ni kuhakikisha inajenga, kuendeleza na kusimamia bandari zote nchini.