Nahodha wa Al-Nassr, Cristiano Ronaldo, ameripotiwa kuwasiliana na wapinzani wa Real Madrid wa Ligi Kuu ya Uhispania La Liga Atletico Madrid kuhusu uhamisho wa kwenda Uhispania.
Ronaldo anataka kuondoka Saudi Arabia, miezi michache tu baada ya kujiunga na Al-Nassr kwa uhamisho wa bure.
Kulingana na ripoti ya El Nacional, fowadi huyo wa zamani wa Manchester United hana furaha Mashariki ya Kati na anatafuta njia ya kutoroka.
Nahodha huyo wa Ureno ameamua kwamba anataka kurejea Ulaya kwa sababu za nje ya uwanja na anaitolea macho Atletico Madrid.
Atletico Madrid ilimtoa kwa mkopo Joao Felix kwenda Chelsea, na ripoti zinaonyesha kuwa wababe hao wa Premier League wako tayari kumbakisha kwa kudumu. Rojablancos pia walimruhusu Matheus Cunha ajiunge na Wolves na sasa wanatafuta washambuliaji.
Hata hivyo, ripoti hiyo iliongeza kuwa Ronaldo anataka kutumia fursa hiyo na anashinikiza kujiunga na Atletico Madrid msimu huu wa joto.