Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Daniel Chongolo amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Iringa Halima Dendegu kuhakikisha mpaka kufikia Julai Mosi mwaka huu kituo cha afya cha Banda Bichi kiwe kimefunguliwa na kuanza kutoa huduma kwa wananchi.
Aidha Chongolo amesema kufikia Julai Mosi atahakikisha Halmashauri ya Wilaya ya Iringa inakabidhiwa gari tatu ,mbili za kubeba wagonjwa na moja ya kufatilia shughuli mbalimbali ikiwemo ukaguzi.
Ametoa agizo hilo Mei 29,2023 alipokuwa akizungumza na wananchi baada ya kushiriki Mkutano Kwa Balozi wa Shina Na. 04 Kata ya Ifunda katika halmashauri ya wilaya ya Iringa, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku saba ya kukagua uhai wa chama na utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025.
Amesema haiwezekani Serikali ijenge majengo mazuri na yenye vifaa vya kisasa lakini hakuna huduma zinazotolewa kwa wananchi kitu ambacho hawezi kukubaliana nacho kama mtendaji mkuu wa chama.
Aidha Chongolo amemuagiza Meneja wa Mamlaka ya Maji Safi na Mazingira vijijini Joyce Bahati kuhakikisha mpaka kifikia desemba 31,2023 maji safi na salama katika kata ya ifunda yanatoka ili wananchi wasiendelee kuhangaika kufata maji mwendo mrefu.