Hadi kufikia Mei, mwaka huu Bandari ya Dar es Salaam imeweza kuhudumia shehena ya mzigo mbalimbali zaidi ya tani milioni 18 kutoka kwenye lengo lililowekwa la kuhudumia tani milioni 19.6 za shehena.
Kwa muda uliobaki, uko uwezekano mkubwa wa kuvuka lengo hadi kufikia kuhudumia tani milioni 20 za shehena jambo ambalo halijawahi kutokea tangu kuanzishwa kwa bandari hiyo.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam Mrisho Mrisho akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake kuhusu maboresho yaliyofanywa pamoja na utendaji kazi wa bandari hiyo.
Mrisho amesema, bandari hiyo imepita katika michakato mbalimbali ya maboresho kwa lengo la kuongeza ufanisi ikiwemo kuhudumia shehena kwa siku chache zaidi na kutatua changamoto zilizokuwepo.
Ameongeza kuwa, kufuatia maboresho makubwa yaliyofanyika katika bandari hiyo ikiwemo ujenzi wa gati mpya tatu (03), kuongeza kina cha maji kutoka mita 6-7 hadi mita 14.5 na kuboresha magati yaliyokuwepo awali, hali ambayo pamoja na mambo mengine imepunguza muda wa kuhudumia shehena ambapo kwa sasa muda wa kuhudumia shehena hauzidi siku nne.
“Baada ya maboresho katika bandari ya Dar es Salaam Kina cha maji kimeongezeka kutoka mita 6-7 hadi kufikia mita 14.5 na kuwezesha meli kuhudumiwa katika gati lolote ndani ya bandari na bandari ya Dar es Salaam, hatua hii imefanya kuwa na idadi kubwa ya meli zinazohudumiwa katika bandari hii” alisema Mrisho
Kufuatia maboresho hayo, Mrisho ameeleza kuwa, moja ya matokeo chanya yaliyoonekana ni pamoja kuongezeka kwa idadi kubwa ya meli kubwa (Deep sea vessel) zaidi ya 90 kuhudumiwa ndani ya mwezi mmoja.
“Watumiaji wa bandari ya Dar es Salaam wameongezeka sana, hivi sasa kwa mwaka mmoja tu tunahudumia magari kati ya 250,000 hadi 300,000, na 60% ya magari hayo ni ya nchi jirani” alisisitiza Mrisho
Ameendelea kwa kusema kuwa, kwa sasa katika bandari hiyo kuna gati jipya maalum kwa ajili ya kuhudumia shehena ya magari jambo ambalo limeifanya bandari hiyo kuweka rekodi ya kihistoria kwani hapo awali shehena ya magari ililkwa ikihudumiwa kwa kuchanganywa na shehena nyingine.
Akiongelea dhana ya ushiriki wa sekta binafsi na mchango wake katika shughuli za bandari hususan bandari ya Dar es Salaam, Mkurugenzi Mrisho amesema
“Hakuna namna, na ni lazima kuwe na ushiriki wa sekta binafsi katika uendeshaji wa Bandari, na hii inafanyika duniani kote. Kuna vifaa vya uendeshaji wa bandari ni gharama kubwa na fedha zinatoka serikalini, na wakati huo huo serikali inafanya kazi nyingi ikiwemo ujenzi wa miundombinu mbalimbali ikiwemo madarasa, barabara, miradi ya umeme, maji na vyote hivi hutumia fedha”
Kwa upande wake mdau wa bandari ambaye pia ni Mkurugenzi wa kampuni ya Uwakala ya Epic Mhandisi Tonny Swai, ametoa wito kwa watumiaji wa bandari kutumia bandari za Tanzania kwa kuwa ni salama, unafuu katika gharama na kutumia muda mchache wa kuhudumia shehena.
Mhandisi Swai amesisitiza kuwa, usalama katika bandari ya Dar es Salaam ni wa kiwango cha juu kwa kuwa kamera za usalama zimefungwa kila kona na hivyo hakuna uwezekano hata kidogo wa wizi wowote kufanyika katika bandari hiyo.
Bandari ya Dar es Salaam ni lango la kuu la kibiashara, asilimia 95 ya biashara ya kimataifa ya Tanzania inahudumiwa na bandari hii. Aidha, bandari hii inahudumia nchi jirani zisizo na bandari kama vile Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Burundi, Rwanda, Malawi, Uganda na Zimbabwe.
Bandari ya Dar es salaam ni kiungo kikuu cha kibiashara si tu kutoka na kwenda nchi za Afrika Mashariki na kati, bali pia na nchi za Mashariki ya kati, Mashariki ya mbali, Ulaya, Australia na Marekani.