SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limewataka wananchi kusoma taarifa zilizopo kwenye vifungashio vya bidhaa hususani za vyakula ili kuepuka madhara mbalimbali ya kiafya yanayoweza kujitokeza.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 29,2023 Jijijini Dar es Salaam, Kaimu Meneja wa Ukaguzi na Utekelezaji wa Sheria TBS, Bw. Moses Mbambe amesema kuna umuhimu mkubwa wananchi wakawa wanasoma taarifa kwenye vifungashio vya chakula kwani inasaidia kuelewa matumizi sahihi ya chakula kilichomo ndani ya kifungashio bila kuleta madhara.
“Wananchi wengi wamekuwa hawatengi muda wa kusoma zile taarifa zilizopo kwenye vifungashio, tumekuwa tukipokea malalamiko ya wateja, amenunua chakula fulani baada ya kukitumia akajikuta amepata madhara ya kiafya lakini aliposoma taarifa zile za kifungashio anakuta chakula kilikuwa kimekwisha muda wake wa matumizi”. Amesema
Pamoja na hayo amesema suala la uwekaji wa taarifa za lebo kwenye vifungashio ni suala muhimu na vilevile ni suala la kisheria ambalo linawataka wazalishaji wa vyakula vilivyofungashiwa kuweka taarifa zao kwenye vifungashio vyao kwa mujibu wa kiwango cha chakula husika.
Amesema kinywaji cha Energy Drink kimekuwa kikileta matatizo ya kiafya hasa ya moyo kwa wanywaji wa kinywaji hicho kwasababu ya uwepo wa kiwango kikubwa cha Caffeine ndo maana kwenye taarifa zilizopo kwenye lebo ya kifungashio cha kinywaji hicho imeelezwa kiwango cha utumiaji kwa siku na ni vyema watumiaji wakazingatia maelekezo
“Kwenye kopo moja la kinywaji hiki wakati mwingine inakuwa na caffeine isiopungua miligramu 500, ukiinywa nyingi inaweza kukuletea madhara ya kiafya kwasababu unakunywa kinywaji kingi kuliko kile ambacho kimewekwa kikomo kwa siku”. Ameeleza
Hata hivyo amesema watumiaji wa chakula wanapokutana na bidhaa ambazo hazijakidhi matakwa ya ubora kwa maana ya bidhaa ambazo zimekwisha muda wa matumizi, wanaweza kupeleka taarifa Makao Makuu ya TBS au kufika moja kwa moja katika ofisi za TBS za Kanda ambazo zipo karibu nawe.