Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) imetoa msaada wa vitanda 15 vya kujifungulia katika wodi ya wajawazito Hospitali ya rufaa ya Temeke ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za kuweka mazingira bora na salama kwa mama anapojifungua.
Vitanda hivyo venye thamani ya Sh21 milioni ni sehemu ya ahadi ya TPA kuisaidia hospitali hiyo inayohudumia wastani wa wanawake 20 hadi 30 kwa siku.
Mganga mfawidhi wa hospitali hiyo Dk Joseph Kimaro amesema msaada huo utawapunguzia adha ya kutumia vitanda chakavu na kuboresha mazingira ya chumba cha kujifungulia.
“Wanawake 20 hadi 30 wanajifungua katika hospitali ya Temeke kila siku, kwahiyo vitanda hivi ni hitaji kubwa na vitasaidia kutuwezesha kuviondoa vile vilivyochoka,” amesema na kuongeza;
“Kitanda kilicho madhubuti kina mchango mkubwa katika kuhakikisha mama anajifungua salama, hii inaakisi ile dhana ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kampeni yake ya Pamoja Tuwavushe Salama,” amesema Dk Kimaro.
Akizungumza kwa niaba ya TPA makao makuu, Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam Mrisho Mrisho amesema mamlaka hiyo itaendelea kuwa sehemu ya taasisi zinazosaidia sekta ya afya hususani kuwezesha uboreshaji wa huduma katika hospitali hiyo iliyo jirani na eneo la bandari.
Pamoja na vitanda, Mrisho ameahidi kuwa bandari itaisaidia hospitali hiyo kupata gari kwa ajili ya kitengo cha ukusanyaji damu kwa ajili ya kukusanya damu na kutengeneza bidhaa za damu.
Akipokea msaada huo Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Mwanahamisi Munkunda ameiomba TPA kuendelea kuishika mkono hospitali hiyo inayotegemewa na wakazi wa wilaya hiyo.