Vyama vya upinzani nchini Uganda vinataka katiba ya nchi hiyo pamoja na sheria za uchaguzi vifanyiwe mageuzi kabla ya uchaguzi mkuu mwaka 2026.
Kulingana na wanasiasa wa upinzani, Uganda haiwezi kudai kutawaliwa kidemokrasia katika mazingira ya sasa ambapo katiba imefanyiwa mageuzi kwa ajili ya kuendeleza utawala wa Rais Yoweri Museveni. Museveni ametawala nchi hiyo tangu mwaka 1986.
Viongozi na wabunge wa vyama vya siasa vya upinzani wameshiriki mkutano wa siku tatu kujadili mapendekezo wanayotaka kuwasilisha bungeni ili kuboresha utawala wa kidemokrasia Uganda.
Wakiongozwa na Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine na Dkt Kizza Besigye, wanasiasa wa upinzani wametoa angalizo kuwa pana haja ya dharura kuhakikisha kuwa katiba ya nchi pamoja na sheria za uchaguzi vinachunguzwa upya.
Wabunge wa upinzani watawasilisha mapendekezo ya kuifanyia mageuzi katiba ya nchi wakitaka awamu mbili za utawala wa rais zirejeshwe. Aidha wanataka umma uhusishwe katika kuwachuja majaji na maafisa wa tume ya uchaguzi kabla ya kuteuliwa katika nafasi hizo. Dkt Kizza Besigye ametoa angalizo kuwa hii ni muhimu kwa sababu katika chaguzi ambazo zimefanyika ushindi wa rais Museveni umetangazwa na mahakama wala si kutokana na matokeo ya uchaguzi.