Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Aretas Lyimo amewataka Wanawake wa kitanzania kuwa makini kutokana na Wanaume Raia wa kigeni kubuni mbinu mpya ya kuanzisha mahusiano ya kimapenzi na Wanawake wa kitanzania zaidi ya mmoja na kuficha dawa za kulevya kwenye makazi ya Wanawake hao huku wao wakipanga nyumba tofauti na pale dawa zikimamatwa huwakana Wanawake hao.
Akiongea leo Dar es salaam amesema “Kutokana na udhibiti kuwa mkubwa, Wafanyabiashara wa dawa za kulevya wameendelea kubuni mbinu mpya za usafirishaji wa dawa za kulevya ili kukwepa kukamatwa, Mamlaka imebaini mbinu hizo na kuchukua hatua, mbinu mojawapo inayotumika ni Raia wa kigeni mmoja kuanzisha mahusiano ya kimapenzi na Wanake wa kitanzania zaidi ya mmoja na kuficha dawa za kulevya kwenye makazi ya Wanawake hao huku wao wakipanga nyumba tofauti na wanakoishi Wapenzi wao”
“Hali hii husababisha Wanawake wa kitanzania kuingia kwenye matatizo makubwa ya kukamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria huku Wanaume wakiwakana Wanawake hao, Mamlaka imejipanga kikamilifu kupambana na biashara ya dawa za kulevya hivyo wanaojihusisha au wenye mpango wa kujihusisha na biashara hiyo waache mara moja au wajisalimishe wenyewe kabla hawajafikiwa na mkono wa sheria”
“Wananchi wanapaswa pia kuwa makini na mizigo wanayopewa kubeba au kuhifadhi pasipo kujua ndani yake kuna nini, Wanawake wanatakiwa kuwa makini zaidi kwani katika baadhi ya matukio wamekuwa wakitumiwa na Wapenzi wao hasa Raia wa kigeni kusafirisha na kupokea mizigo wasiyoijua na wakati mwingine mizigo hiyo huwa na dawa za kulevya na hivyo hujikuta matatani”